1 Yohana 5

1 Yohana 5

Watoto wa Mungu Ushindeni Ulimwengu

1Watu wanao amini kuwa Yesu ni Masihi ni wana wa Mungu. Na kila ampendae Baba pia anawapenda watoto wa Baba.

2Twatambuaje kuwa tunawapenda watoto wa Mungu? Twatambua kwa sababu tunampenda Mungu na tunazitii amri zake.

3Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na amri za Mungu si ngumu kwetu,

4kwa sababu kila ambae ni mwana wa Mungu ana uwezo wa kushinda dhidi ya ulimwengu. Ni imani yetu iliyoshinda vita dhidi ya ulimwengu.

5Hivyo ni nani anayeushinda ulimwengu? Ni wale tu wanaoamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu.

Mungu alituambia kwa Habari ya Mwanae

6Yesu Kristo ndiye aliyekuja. Alikuja kwa maji na damu. Hakuja kwa maji peke yake. Lahasha, Yesu alikuja kwa vyote maji na damu. Na Roho atuambia kuwa hili ni kweli. Roho ndiye Kweli.[#5:6 Inaweza kumaanisha Maji ya ubatizo wa Yesu Kristo, na damu aliyo imwaga pale msalabani.]

7Kwa hiyo kuna mashahidi watatu wanao tuambia habari za Yesu:

8Roho, Maji, na Damu. Mashuhuda hawa watatu wanakubaliana.

9Tunawaamini watu wanaposema jambo llililo kweli. Lakini kile anachosema Mungu ni muhimu zaidi. Na Hivi ndivyo Mungu alivyotuambia: Alituambia ukweli kuhusu Mwanaye.

10Kila amwaminiye Mwana wa Mungu anayo kweli ambayo Mungu alituambia. Lakini watu wasiomwamini Mungu wanamfanya Mungu kuwa mwongo, kwa sababu hawaamini kile ambacho Mungu ametueleza kuhusu mwanaye.

11Hiki ndicho ambacho Mungu alitueleza: Mungu ametupatia uzima wa milele, na uzima huu umo katika wanawake.

12Yeyote aliye na mwana anao uzima wa milele, lakini asiye na mwana wa mungu hana huo uzima wa milele.

Tunao uzima wa Milele Sasa

13Ninawaandikia barua hii ninyi mnaomwamini Mwana wa Mungu ili mjue ya kwamba sasa mnao uzima wa milele.

14Tunaweza kwenda kwa Mungu tukiwa na ujasiri huo. Hii ina maana kuwa tunapomwomba Mungu mambo (na mambo hayo yakakubaliana na matakwa yake kwetu), Mungu huyajali yale tunayosema.

15Hutusikiliza kila wakati tunapomwomba. Hivyo tunatambua kuwa yeye hutupa kila tunachomwomba.

16Utakapomwona muumini mwenzio akitenda dhambi (Dhambi isiyomwongoza kwenye mauti), unapaswa kumwombea. Kisha Mungu atampa uzima. Ipo aina ya dhambi inayomwongoza mtu hadi mauti ya milele. Sina maana ya kusema unapaswa kuombea aina hiyo ya dhambi.

17Daima kutenda yasiyo haki ni dhambi. Lakini ipo dhambi isiyomwongoza mtu katika mauti ya milele.

18Tunajua kwamba wale waliofanyika watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi. Mwana wa Mungu anawahifadhi salama. Yule Mwovu hawezi kuwagusa.[#5:18 Kwa maana ya kawaida, “Yeye aliye aliyezaliwa kutokana na Mungu hutunzwa” au “anajitunza”.]

19Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, Lakini yule Mwovu anautawala ulimwengu wote.

20Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupa uelewa. Hivyo sasa tunaweza kumjua yeye aliye kweli, na tunaishi katika Mungu huyo wa kweli. Nasi tumo ndani ya mwanaye, Yesu Kristo. Yeye ndiye Mungu wa kweli, naye ndiye uzima wa milele.

21Kwa hiyo, watoto wapendwa, mjiepushe na miungu wa uongo.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International