The chat will start when you send the first message.
1Mimi, Paulo, ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo. Wengine wanasema kuwa nina ujasiri ninapowaandikia nikiwa mbali, lakini ni mwoga kusema jambo lo lote ninapokuwa pamoja nanyi.
2Wanadhani sababu ya kutenda yale tunayoyafanya ni kama zile za kidunia. Ninapanga kuwa jasiri sana kinyume chao watu hao hapo ninapokuja kwenu. Tafadhali ninawaomba, sitahitaji kutumia ujasiri huo kwenu.
3Tunaishi katika ulimwengu huu, lakini hatupigani vita yetu kama ulimwengu unavyopigana.
4Silaha tunazozitumia si za kibinadamu. Silaha zetu zina nguvu kutoka kwa Mungu na zinaweza kuharibu ngome za adui. Tunaharibu mabishano ya watu,
5na tunasambaratisha kila wazo la kiburi linalojiinua kinyume cha elimu ya Mungu. Pia tunateka kila wazo na kulitiisha ili limtii Kristo.
6Tuko tayari kumwadhibu kila mtu asiyetii, lakini tunataka ninyi muwe watiifu ipasavyo kwanza.
7Mnatakiwa kuchunguza ukweli halisi wa mambo ulio mbele ya macho yenu. Ikiwa mna uhakika kuwa ninyi ni wa Kristo, mnapaswa kukumbuka kuwa na sisi ni wa Kristo kama ninyi mlivyo wa Kristo.
8Inaweza kuonekana kana kwamba tunajivuna sana kupita kiasi kidogo kuhusu mamlaka ambayo Bwana ametupa sisi. Lakini alitupa mamlaka hii ili kuwatia nguvu ninyi, na sio kuwaumiza. Hivyo sitaona haya kwa lolote ambalo tumejisifu kwalo.
9Sitaki mfikiri kuwa najaribu kuwatisha kwa barua zangu.
10Wengine wanasema, “Barua za Paulo zina shuruti na matakwa mengi, Lakini anapokuwa pamoja nasi, ni mdhaifu na msemaji asiyefaa.”
11Watu hao wanapaswa kulielewa jambo hili: tutakapokuwa pamoja nanyi, tutatenda mambo kwa ujasiri ule ule tunaouonyesha sasa katika barua zetu.
12Hatujaribu kujiweka katika daraja moja na wale wanaojisifu wenyewe. Hatujilinganishi na watu hao. Wao wanatumika wenyewe kwa kujipima wenyewe, na wanajilinganisha miongoni mwao wenyewe. Hili linadhihirisha kuwa hawajui lolote.
13Lakini hatutajisifia lolote nje ya kazi tuliyopewa kuifanya. Tutaweka ukomo wa kujisifia kwetu katika kazi aliyotupa Mungu kuifanya, lakini kazi hii inajumuisha kazi yetu kwenu.
14Tungekuwa tunajivuna zaidi na zaidi ikiwa tungekuwa hatujafika kabisa kwenu. Lakini tulikuwa wa kwanza kufika kwenu na Habari Njema ya Kristo.
15Tumeweka ukomo wa kujivuna kwetu katika kazi ambayo ni yetu. Hatujivunii kazi ambayo wameifanya watu wengine. Tunatumaini kuwa imani yenu itaendelea kukua. Tunatumaini kuwa mtaisadia kazi yetu kukua zaidi na zaidi.
16Tunataka kuieneza habari njema katika maeneo ya mbali zaidi kupita mji wenu. Hatutaki kujisifia juu ya kazi ambayo imefanywa na mtu mwingine katika eneo lake.
17“Yeyote anayejisifu na ajisifu juu ya Bwana tu.”[#Yer 9:24]
18Kile watu wanachosema kuhusu wao wenyewe hakina maana yeyote. Cha muhimu ni ikiwa Bwana anasema kuwa wamefanya vizuri.