3 Yohana 1

3 Yohana 1

1Salamu toka kwa mzee.[#1:1 Huyu huenda alikuwa ni Mtume Yohana. “Mzee” ina maana ya mtu aliye mtu mzima au kiongozi maalumu katika kanisa (kama vile katika Tit 1:5).]

Kwa rafiki mpendwa gayo, mtu ni mpendae kwa dhati.

2Rafiki yangu mpendwa, najua kwamba unaendelea vizuri kiroho, kwa hiyo ninaomba kuwa mengine yote yaendelee vizuri pia nawe uwe na afya njema.

3Baadhi ya waamini walikuja na kunieleza juu ya kweli iliyo katika maisha yako. Waliniambia kuwa unaendelea kuifuata njia ya kweli. Hili lilinifanya nijisikie furaha sana.[#1:3 Kweli au “habari njema” za Yesu Kristo zinazo waunganisha waamini wote pamoja. Pia katika mstari wa 8,12.]

4Daima hili hunipa furaha iliyo kuu ninaposikia kuwa wanangu wanaifuata njia ya kweli.

5Rafiki yangu mpendwa, inapendeza kuwa unaonesha uaminifu wako katika kazi yako yote miongoni mwa waaminio. Wengine ambao huwajui.

6Hao waliliambia kanisa juu ya upendo ulio nao. Tafadhali wasaidie kuendelea na safari yao. Wasaidie katika njia ambayo itampendeza Mungu.

7Safari hiyo waliyoenda ni ya kumtumikia Kristo. Hawakupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini.

8Hivyo inatupasa kuwasaidia. Tunapowasaidia, tunashiriki kazi yao katika ile kweli.

9Niliandika barua kwa kanisa, ila Diotrefe hasikilizi yale tunayosema. Yeye daima anataka kuwa kiongozi.

10Nitakapokuja, nitaongea naye mbele ya kanisa juu ya hiki anachokifanya. Anadanganya na kusema mambo mabaya juu yetu, lakini hayo siyo yote. Anakataa kuwapokea na kuwasaidia wanaoamini wanaosafiri kwenda huko. Na hawaruhusu watu wengine kuwasaidia. Kama wakifanya hivyo, anawazuia wasikusanyike na kanisa tena.

11Rafiki yangu mpendwa, usiige lililo baya; bali iga lililo jema. Yeyote anayetenda yaliyo mema hutoka kwa Mungu. Ila yeyote anayetenda maovu bado hajamjua Mungu.

12Kila mtu azungumza yaliyo mema juu ya Demetrio, na kweli inakubaliana na yale wasemayo. Pia, twasema mema juu yake. Na unafahamu kuwa tusemayo ni kweli.

13Nina mambo mengi nataka kukueleza. Lakini sipendi kutumia kalamu na wino.

14Natumaini kukutembelea hivi karibuni. Hapo tunaweza kukaa pamoja na kuongea uso kwa uso.

15Amani kwako. Rafiki walio pamoja nami hapa wakutumia upendo wao. Tafadhali wapatie upendo wetu kila rafiki waliopo huko.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International