Wakolosai 1

Wakolosai 1

1Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka niwe. Salamu pia kutoka kwa Timotheo ndugu yetu katika Kristo.[#1:1 Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32; Lk 23:2. Tazama pia na katika Orodha ya Maneno.]

2Salamu kwenu kaka na dada zetu watakatifu na walio waaminifu katika Kristo mlioko Kolosai.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu ziwe pamoja nanyi.

3Katika maombi yetu tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Yeye ndiye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

4Nasi tunamshukuru Yeye kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu na upendo wenu kwa watu wa Mungu wote.

5Imani yenu na upendo wenu vinatokana na ufahamu kwamba mtapokea kile mnachotumaini. Hicho ambacho Mungu amekihifadhi salama mbinguni kwa ajili yenu. Hilo ni tumaini lile lile ambalo mmekuwa nalo tangu mliposikia kwa mara ya kwanza ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema.

6Habari Njema hii imezaa matunda na imeenea ulimwenguni kote. Na hicho ndicho kilichokuwa kikitokea tangu siku mliposikia kwa mara ya kwanza na kuelewa ukweli wa neema ya Mungu.

7Kweli hiyo mliisikia kutoka kwa Epafra, aliye mtumwa wa Bwana pamoja nasi. Yeye anatusaidia sisi kama mtumishi mwaminifu wa Kristo.[#1:7 Nakala nyingi za kale za Kiyunani zina neno hili “anakusaidia wewe”.]

8Naye ametueleza pia kuhusu upendo mlioupokea kutoka kwa Roho Mtakatifu.

9Ndugu zangu tangu siku tuliposikia mambo haya juu yenu, tumeendelea kuwaombea, na haya ndiyo maombi yetu kwa ajili yenu:

Ndipo nanyi mtakapofurahi,

12na kumshukuru Mungu Baba. Kwani yeye amewastahilisha kupokea kile alichowaahidi watakatifu wake, wanaoishi katika nuru.

13Mungu ametuweka huru kutoka katika nguvu za giza. Naye ametuingiza katika ufalme wa Mwanaye mpendwa.

14Na huyo Mwana amelipa gharama ya kutuweka huru, kwani ndani yake tuna msamaha wa dhambi zetu.

Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu

15Hakuna anayeweza kumwona Mungu,

lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.

Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.

16Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:

vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,

watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.

Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.

17Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,

na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.

18Yeye ni kichwa cha mwili,

yaani kanisa.

Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,

ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.

Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.

19Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake

uishi ndani ya Mwana.

20Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi

kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;

vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.

Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.

21Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye.

22Lakini sasa amewafanya kuwa rafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake;

23na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya.

Kazi ya Paulo kwa Ajili ya Kanisa

24Nina furaha kwa sababu ya mateso ninayopata kwa manufaa yenu. Yapo mambo mengi ambayo kupitia hayo Kristo bado anateseka. Nami ninayapokea mateso haya kwa furaha katika mwili wangu kwa ajili ya mwili wake, yaani Kanisa.

25Nilifanyika kuwa mtumishi wa kanisa kwa sababu Mungu alinipa kazi maalum ya kufanya. Kazi hii inawasaidia ninyi, nayo ni kuuhubiri ujumbe kamili wa Mungu.

26Ujumbe huu ni ukweli wenye siri uliofichwa tangu mwanzo wa nyakati. Nao ulifichwa kutoka kwa kila mtu kwa muda mrefu, lakini sasa umedhihirishwa kwa watakatifu wa Mungu.

27Mungu aliamua kuwajulisha watu wake namna Kweli hii ilivyo na utajiri na utukufu. Siri hii ya kweli hii, ambayo ni kwa ajili ya watu wote, ni kwamba Kristo anaishi ndani yenu. Yeye ndiye tumaini la kushiriki katika utukufu wake.

28Hivyo tunaendelea kuwaambia watu juu ya Kristo. Tunatumia hekima yote kumshauri na kumfundisha kila mtu. Tunajaribu kumleta kila mtu mbele za Mungu kama watu waliokomaa kiroho katika uhusiano wao na Kristo.

29Kwa kufanya hivi, ninafanya kazi kwa bidii, nikijitahidi na kutumia nguvu kubwa aliyonipa Kristo. Nguvu hiyo inafanya kazi katika maisha yangu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International