Waefeso 4

Waefeso 4

Umoja wa Mwili wa Kristo

1Hivyo, mimi niliye mfungwa kwa ajili ya Bwana nawasihi mwishi kwa jinsi inavyowapasa watu wa Mungu, kwa sababu aliwachagua muwe wake.

2Iweni wanyenyekevu na wapole siku zote. Mvumiliane na kuchukuliana ninyi kwa ninyi katika upendo.

3Mmeunganishwa pamoja kwa amani na Roho. Jitahidini mwezavyo kudumu kuutunza umoja huo, mkiunganishwa pamoja kwa amani.

4Kuna mwili mmoja na Roho moja, na Mungu aliwachagua ili muwe na tumaini moja.

5Kuna Bwana mmoja, imani moja, na ubatizo mmoja.

6Mungu ni mmoja na ni Baba wetu sote, anayetawala juu ya kila mtu. Hutenda kazi kupitia kwetu sote na ndani yetu sote.

7Kristo alimpa kila mmoja wetu karama. Kila mmoja alipokea kwa jinsi alivyopenda yeye kuwapa.

8Ndiyo maana Maandiko yanasema,

“Alipaa kwenda mahali pa juu sana;

aliwachukua wafungwa pamoja naye,

na akawapa watu vipawa.”

9Inaposema, “Alipaa juu,” inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa kwanza alikuja chini duniani.

10Hivyo Kristo alishuka chini, na ndiye aliyekwenda juu. Alikwenda juu ya mbingu za juu zaidi ili avijaze vitu vyote pamoja naye.

11Na Kristo huyo huyo aliwapa watu hawa vipawa: aliwafanya wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kwenda na kuhubiri Habari Njema, na wengine kuwa wachungaji ili wawafundishe watu wa Mungu.[#4:11 Kwa maana ya kawaida “kuwahudumia na kuwafundisha watu”.]

12Mungu aliwapa hao ili kuwaandaa watakatifu wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma, kuufanya imara mwili wa Kristo.

13Kazi hii inabidi iendelee hadi wote tutakapounganishwa pamoja katika lile tunaloliamini na tunalolijua kuhusu Mwana wa Mungu. Lengo letu ni kufanana na mtu mzima aliyekomaa na kuwa kama Kristo tukiufikia ukamilifu wake wote.

14Ndipo tutakapokuwa si kama watoto wachanga. Hatutakuwa watu ambao nyakati zote hubadilika kama meli inayochukuliwa na mawimbi huku na kule. Hatutaweza kuathiriwa na fundisho lolote jipya tutakalosikia kutoka kwa watu wanaojaribu kutudanganya. Hao ni wale wanaoweka mipango ya ujanja na kutumia kila aina ya mbinu kuwadanganya wengine waifuate njia iliyopotoka.

15Hapana, tunapaswa kusema ukweli kwa upendo. Tutakua na kuwa kama Kristo katika kila njia. Yeye ni kichwa,

16na mwili wote unamtegemea yeye. Viungo vyote vya mwili vimeunganishwa na kushikanishwa pamoja, huku kila kiungo kikitenda kazi yake. Hili huufanya mwili wote ukue na kujengeka katika upendo.

Mnavyopaswa Kuishi

17Nina kitu cha kuwaambia kutoka kwa Bwana. Ninawaonya: Msiendelee kuishi kama wale wasiomwamini Mungu wetu. Mawazo yao hayafai kitu.

18Hawana ufahamu, na hawajui lolote kwa sababu wamekataa kusikiliza. Hivyo hawawezi kupata maisha mapya Mungu anayowapa watu.

19Wamepoteza hisia zao za aibu na wanayatumia maisha yao kutenda yale yaliyo mabaya kimaadili. Zaidi ya hapo wanataka kutenda kila aina ya uovu.

20Lakini aina hiyo ya maisha haiko kama ile mliyojifunza mlipomjua Kristo.

21Najua kwamba mlisikia juu yake, na ndani yake mlifundishwa ukweli. Ndiyo, ukweli umo ndani ya Yesu.

22Mlifundishwa kuacha utu wenu wa kale. Hii inamaanisha kwamba mnapaswa kuacha kuishi katika njia za uovu mlivyoishi zamani. Utu wenu wa kale huharibika zaidi na zaidi, kwa sababu watu hudanganywa na uovu wanaotaka kuutenda.

23Mnapaswa kufanywa upya katika mioyo yenu na katika fikra zenu.

24Kila mmoja wenu auvae utu ule mpya ulioumbwa kwa kufananishwa na Mungu, ambao kwa hakika una wema na ni wenye kumpendeza Mungu.

25Hivyo mnapaswa kuacha kusema uongo, “Nyakati zote mseme ukweli tu,” kwa sababu wote sisi tunahusiana na ni wa mwili mmoja.[#Zek 8:16]

26“Unapokasirika, usiruhusu hasira hiyo ikusababishe wewe kutenda dhambi,” na usiendelee na hasira kwa siku nzima.[#Zab 4:4 (Tafsiri ya Kiyunani)]

27Usimwachie Ibilisi nafasi ya kukushinda.

28Yeyote ambaye amekuwa akiiba anapaswa kuacha kuiba na afanye kazi. Unapaswa kutumia mikono yako kufanya kitu chenye kufaa. Hapo utakuwa na kitu cha kuwashirikisha walio maskini.

29Unapozungumza, usiseme chochote kilicho kibaya. Bali useme mambo mazuri ambayo watu wanayahitaji ili waimarike. Ndipo kile unachosema kitakuwa ni baraka kwa wale wanaokusikia.

30Tena usimhuzunishe Roho Mtakatifu. Mungu alikupa Roho Mtakatifu kama uthibitisho kwamba wewe ni wake na kwamba atakulinda hadi siku atakapokufanya uwe huru kabisa.

31Usiwe na uchungu, wala kukasirika. Kamwe usiongee kwa hasira au kusema chochote ili uwaumize wengine. Usifanye chochote kilicho kiovu.

32Muwe mwema na mpendane ninyi kwa ninyi. Msameheane ninyi kwa ninyi kama Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International