The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni. Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.[#14:1 Jina jingine la Yerusalemu, hapa limetumika kumaanisha mji wa kiroho ambamo watu wa Mungu wanaishi pamoja naye.]
2Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao.
3Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua.
4Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake. Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo.[#14:4 Ubikira au kuwa safi dhidi ya zinaa ni ishara ya kuwa na imani kwa Mungu kwa kupinga majaribu na kila aina ya ibada ya sanamu.]
5Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa.
6Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi.
7Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”
8Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”
9Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao.
10Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu. Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo.[#14:10 Wayunani na Warumi wa kale walikuwa na kawaida ya kunywa mvinyo uliochanganywa na maji. Anachokisema malaika hapa ni kwamba mvinyo huu wa ghadhabu ya Bwana umemwagwa pasipo kuchanganywa na maji. Ni mvinyo ulio na nguvu yake yote pasipo kulainishwa na maji.]
11Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.”
12Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.
13Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”
Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”
14Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake.
15Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.”
16Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.
17Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali.
18Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.”
19Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu.
20Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[#14:20 Kwa maana ya kawaida, “ 1,600”.]