Ufunuo 17

Ufunuo 17

Mwanamke Juu ya Mnyama Mwekundu

1Mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli sa akaja kuzungumza nami. Akasema, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu itakayotolewa kwa kahaba maarufu. Ndiye yule aketiye juu ya maji mengi.

2Watawala wa dunia walizini pamoja naye. Watu wa dunia walilewa kutokana na mvinyo wa dhambi yake ya uzinzi.”

3Kisha malaika akanichukua mbali kwa Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke amekaa juu ya mnyama mwekundu. Mnyama alikuwa ameandikwa majina ya kumkufuru Mungu katika mwili wake wote. Alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.

4Mwanamke aliyekuwa juu yake alikuwa amevaa nguo za zambarau na nyekundu. Alikuwa anang'aa kutokana na dhahabu, vito na lulu alizokuwa amevaa. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu. Kikombe hiki kilijaa maovu na machukizo ya dhambi yake ya uzinzi.

5Alikuwa na jina kwenye kipaji cha uso wake. Jina hili lina maana iliyofichwa. Hiki ndicho kilichoandikwa:

6Nikatambua kuwa mwanamke alikuwa amelewa. Alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu wa Mungu. Alikuwa amelewa kwa damu ya wale walioshuhudia imani yao katika Yesu Kristo.

Nilipomwona mwanamke, nilishangaa sana.

7Kisha malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Nitakuambia maana iliyofichwa kuhusu mwanamke huyu na mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumi anayeendeshwa na mwanamke huyu.

8Mnyama unayemwona alikuwa hai kwanza, lakini sasa si hai. Hata hivyo, atapanda kutoka kuzimu na kwenda kuangamizwa. Watu wanaoishi duniani watashangaa watakapomwona mnyama, kwa sababu aliwahi kuwa hai, hayuko hai, lakini atakuwa hai tena. Hawa ni watu ambao majina yao hayajawahi kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu.

9Unahitaji hekima kulielewa hili. Vichwa saba juu ya mnyama ni milima saba ambako mwanamke amekaa. Pia ni watawala saba.

10Watawala watano wamekwisha kufa tayari. Mmoja wa watawala anaishi sasa, na mtawala wa mwisho anakuja. Atakapokuja, atakaa kwa muda mfupi tu.

11Mnyama ambaye hapo kwanza alikuwa hai, lakini haishi tena ni mtawala wa nane. Naye ni mmoja wa watawala saba wa kwanza. Naye ataangamizwa.

12Pembe kumi ulizoziona ni watawala kumi. Watawala hawa kumi hawajapata falme zao, lakini watapata nguvu ya kutawala pamoja na mnyama kwa saa moja.

13Lengo la watawala hawa wote kumi linafanana. Nao watampa mnyama nguvu na mamlaka yao.

14Watafanya vita kinyume na Mwanakondoo. Lakini Mwanakondoo atawashinda, kwa sababu ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Pamoja naye watakuwepo wateule wake na wafuasi waaminifu, watu aliowaita kuwa wake.”

15Kisha malaika akaniambia, “Uliyaona maji ambako kahaba amekaa. Maji haya ni watu wengi, wa asili, mataifa, na lugha tofauti ulimwenguni.

16Mnyama na pembe kumi ulizoziona watamchukia kahaba. Watachukua kila kitu alichonacho na kumwacha akiwa uchi. Watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto.

17Mungu aliweka wazo katika akili zao kutenda yale yatakayotimiza kusudi lake. Walikubaliana kumpa mnyama nguvu zao kutawala mpaka yale aliyosema Mungu yamekamilika.

18Mwanamke uliyemwona ni mji mkuu ambao unatawala juu ya wafalme wa dunia.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International