Ufunuo 21

Ufunuo 21

Yerusalemu Mpya

1Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu na dunia ya kwanza vilikwisha kutoweka. Na sasa bahari haikuwepo.

2Nikauona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyevalishwa kwa ajili ya mumewe.[#21:2 Mji wa kiroho ambako Mungu ataishi pamoja na watu wake.]

3Nikasikia sauti kuu kutoka kwenye kiti cha enzi. Ikisema, “Makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Yeye ataishi pamoja nao. Na wao watakuwa watu wake. Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao naye atakuwa Mungu wao.

4Atafuta kila chozi kutoka machoni mwaona. Hakutakuwa na kifo tena, huzuni, kilio wala maumivu. Namna zote za zamani zimepita.”

5Aliyekaa kwenye kiti cha enzi akasema, “Tazama, sasa ninakiumba kila kitu upya!” Kisha akasema, “Andika hili, kwa sababu maneno haya ni kweli na ya kuaminiwa.”

6Akaniambia, “Imekwisha! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Kila mwenye kiu nitampa bure maji kutoka kwenye chemichemi ya maji ya uzima.[#21:6 Herufi ya kwanza na ya mwisho katika mfumo wa herufi wa Kiyunani, hapa inamaanisha “wa Kwanza na wa Mwisho”. Pia katika 22:13.]

7Wale wote watakaoshinda watapokea yote haya. Na nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watoto wangu.

8Lakini waoga, wanaokataa kuniamini, wafanyao mambo ya kuchukiza, wauaji, wazinzi, wachawi, waabuduo sanamu na waongo, nitawatupa katika ziwa linalowaka moto. Hii ni mauti ya pili.”

9Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.”

10Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu.

11Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo.

12Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli.

13Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi.

14Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.

15Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake.

16Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400, upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400.[#21:16 Kwa maana ya kawaida, “ 12,000”.]

17Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60 kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.)[#21:17 Sawa na dhiraa 144 ama futi 197. Dhiraa moja ni urefu wa mkono wa mtu kuanzia kwenye kiwiko cha mkono mpaka kwenye nje ya kidole kidogo, kama nusu mita.]

18Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo.

19Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi,

20la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto.

21Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo.

22Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji.

23Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji.

24Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule. Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji.[#21:24 Yaani, “Mwanakondoo”.]

25Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko.

26Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji.

27Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International