Ufunuo 5

Ufunuo 5

Nani anaweza kukifungua kitabu?

1Kisha niliona kitabu katika mkono wa kulia wa aliyekaa kwenye kiti cha enzi. Kitabu hiki kilikuwa na maandishi pande zote na kilikuwa kimefungwa kwa mihuri saba.[#5:1 Hapa inamaanisha hati ndefu ya kukunja kwa kuvingirisha (ni vitabu vilivyotumika zamani). Katika Biblia unapoona neno kitabu au vitabu, inamaanisha hati hizi.]

2Na nikamwona malaika mwenye nguvu, aliyeita kwa sauti kubwa, “Ni nani anayestahili kuivunja mihuri na kukifungua kitabu?”

3Lakini hakukuwa yeyote mbinguni au duniani au chini ya dunia ambaye angeweza kukifungua kitabu na kutazama ndani yake.

4Nililia sana kwa sababu hakuwepo aliyestahili kukifungua kitabu na kuangalia ndani yake.

5Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie! Simba kutoka kabila la Yuda ameshinda. Ni mzaliwa wa Daudi. Anaweza kukifungua kitabu na mihuri yake saba.”[#5:5 Imetumika hapa kumaanisha Yesu.]

6Kisha nikamwona Mwanakondoo amesimama katikati karibu na kiti cha enzi kilichozungukwa na viumbe wanne wenye uhai. Wazee pia walikuwa wamemzunguka Mwanakondoo aliyeonekana kama aliyeuawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambayo ni roho saba za Mungu zilizotumwa ulimwenguni kote.

7Mwanakondoo alikuja na akakichukua kile kitabu kutoka katika mkono wa kulia wa yule aliyeketi kwenye kiti enzi.

8Baada ya Mwanakondoo kukichukua kile kitabu, viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama mbele za Mwanakondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi. Pia walikuwa wameshikilia bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni maombi ya watu watakatifu wa Mungu.

9Na wote walimwimbia wimbo mpya Mwanakondoo:

“Unastahili kukichukua kitabu

na kuifungua mihuri yake,

kwa sababu uliuawa,

na kwa sadaka ya damu yako uliwanunua watu kwa ajili ya Mungu,

kutoka kila kabila, lugha, rangi na taifa.

10Uliwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa ajili ya Mungu wetu.

Nao watatawala duniani.”

11Kisha, nilipotazama, nikasikia sauti ya malaika wengi waliozunguka kiti cha enzi pamoja na viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne. Walikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika, elfu kumi mara elfu kumi.

12Kwa sauti kuu malaika walisema:

“Mamlaka yote, utajiri, hekima na nguvu ni kwa Mwanakondoo aliyeuawa.

Anastahili kupokea heshima, utukufu na sifa!”

13Ndipo nikasikia kila kiumbe kilichoumbwa kilichoko mbinguni na duniani na chini ya dunia na baharini, viumbe vyote sehemu hizo vikisema:

“Sifa zote na heshima

na utukufu na nguvu kuu ni kwa ajili yake Yeye aketiye

kwenye kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo milele na milele!”

14Viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” Na wazee wakainama chini wakasujudu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International