The chat will start when you send the first message.
1Kisha nilitazama Mwanakondoo alipokuwa anaufungua muhuri wa kwanza kati ya mihuri saba. Kisha nikasikia sauti ya mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ngurumo ya radi ikisema, “Njoo!”[#6:1 Au “chapa maalumu”. Pia katika mstari wa 3.]
2Nilipotazama nilimwona farasi mweupe mbele yangu. Mwendesha farasi aliyekuwa amempanda farasi huyo alikuwa na upinde na alipewa taji. Alimwendesha farasi akatoka kwenda kumshinda adui na ili kupata ushindi.
3Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa pili, nilimsikia kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!”
4Nilipotazama nilimwona farasi mwekundu akitokea. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alipewa mamlaka ya kuondoa amani duniani ili watu wauane. Alipewa upanga mkubwa.
5Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tatu. Nilisikia kiumbe mwenye uhai wa tatu akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweusi mbele yangu. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alikuwa na mizani mkononi mwake.
6Kisha nilisikia kitu kilichosikika kama sauti ikitokea pale walipokuwa viumbe wenye uhai wanne. Kikisema, “Kilo moja ya ngano au kilo tatu ya shayiri itagharimu mshahara wote wa siku moja. Lakini usiharibu upatikanaji wa mafuta ya mzeituni na divai!”[#6:6 “Kibaba au ,” kiasi cha gawio la nafaka kwa ajili ya askari. Ni kama kilo moja.]
7Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa nne nilisikia sauti ya kiumbe wa nne mwenye uhai akisema, “Njoo!”
8Nilipotazama nilimwona farasi mwenye rangi ya kijivu. Aliyempanda alikuwa mauti na kuzimu ilikuwa inamfuata nyuma yake kwa karibu. Alipewa mamlaka juu ya robo ya dunia kuwaua watu kwa upanga, njaa, magonjwa na kwa wanyama wa porini waliomo duniani.
9Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tano, niliziona baadhi ya roho za wale waliokuwa waaminifu kwa neno la Mungu na kweli waliyopokea zikiwa chini ya madhabahu.
10Roho hizi zilipiga kelele kwa sauti kuu zikisema, “Mtakatifu na Bwana wa kweli, ni lini utakapowahukumu watu wa dunia na kuwaadhibu kwa kutuua sisi?”
11Kisha kila mmoja wao alipewa kanzu ndefu nyeupe. Wakaambiwa wasubiri kwa muda mfupi kwani bado walikuwepo ndugu zao katika utumishi wa Kristo ambao ni lazima wauawe kama wao. Roho hizi ziliambiwa zisubiri mpaka mauaji yote yatakapokwisha.
12Kisha nilitazama wakati Mwanakondoo anaufungua muhuri wa sita. Kulitokea tetemeko kubwa la ardhi na jua likawa jeusi kama gunia jeusi na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu.[#6:12 Gunia lililofumwa kwa nyuzi za manyoya maeusi.]
13Nyota zikaanguka chini duniani kama mtini uangushavyo tini zake upepo unapovuma.
14Anga iligawanyika katikati na pande zote zikajiviringa kama kitabu. Na kila mlima na kisiwa kiliondolewa mahali pake.[#6:14 Hapa inamaanisha hati ndefu ya kukunja kwa kuvingirisha (vitabu vilivyotumika zamani). Katika Biblia unapoona neno kitabu au vitabu, inamaanisha hati hizi.]
15Kisha watu wote wa ulimwengu, wafalme, watawala, makamanda wa majeshi, matajiri, wenye mamlaka na nguvu, kila mtumwa na asiye mtumwa, walijificha katika mapango na nyuma ya miamba milimani.
16Waliiambia milima na miamba, “Tuangukieni. Tuficheni mbali na uso wa yule aketiye kwenye kiti cha enzi. Tuficheni dhidi ya hasira ya Mwanakondoo!
17Siku kubwa ya hasira yao imefika. Hakuna anayeweza kupingana nayo.”