The chat will start when you send the first message.
1Malaika wa tano alipopuliza tarumbeta yake, niliiona nyota ikianguka kutoka angani mpaka duniani. Nyota ilipewa ufunguo wa kufungulia shimo refu sana liendalo kuzimu.
2Kisha nyota ikafungua shimo refu sana liendalo kuzimu. Moshi ukatoka kwenye shimo kama moto utokao kwenye tanuru kubwa. Jua na anga vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka kwenye shimo.
3Nzige wakatoka kwenye moshi na wakateremka kwenda duniani. Walipewa nguvu ya kuuma kama nge.
4Waliamriwa kutoharibu nyasi au mimea ya mashambani na mti. Walitakiwa kuwadhuru watu wasio na alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao tu.
5Hawakupewa mamlaka ya kuwaua lakini kuwatia maumivu kwa muda wa miezi mitano, maumivu kama ambayo mtu huyasikia anapoumwa na nge.
6Siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakiona. Watataka kufa, lakini kifo kitajificha.
7Nzige hao walionekana kama farasi walioandaliwa kwa ajili ya mapigano. Vichwani mwao walivaa kitu kilichoonekana kama taji ya dhahabu. Nyuso zao zilionekana kama nyuso za wanadamu.
8Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake. Meno yao yalikuwa kama meno ya simba.
9Vifua vyao vilionekana kama ngao za chuma. Sauti zilizotoka katika mbawa zao zilikuwa kama za farasi wengi na magari ya farasi yaendayo vitani.
10Walikuwa na mikia kama ya nge. Nguvu ya kuwasababishia wanadamu maumivu kwa miezi mitano ilikuwa kwenye mikia yao.
11Walikuwa na mtawala, aliyekuwa malaika wa kuzimu. Jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni. Na kwa Kiyunani ni Apolioni.[#9:11 Ni jina la Kiebrania linalomaanisha “kifo” au “maangamizi”, hutumika kama jina la mahali pa kifo. Tazama Ayu 26:6 na Zab 88:11.; #9:11 Jina linalomaanisha “mteketezaji”.]
12Kitisho cha kwanza kimepita sasa. Bado vinakuja vitisho vingine viwili.
13Malaika wa sita alipopuliza tarumbeta yake, nilisikia sauti ikitoka katika pembe zilizo katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu.[#9:13 Kama za mnyama.; #9:13 Au “kona”.]
14Ikamwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Wafungue huru malaika wanne waliofungwa pembezoni mwa mto mkuu Frati.”
15Malaika hawa wanne walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hii, siku hii, mwezi na mwaka huu. Malaika waliachwa huru ili waue theluthi moja ya watu duniani.
16Nikasikia kuwa idadi ya askari waliowaendesha farasi walikuwa milioni mia mbili.
17Katika maono yangu, niliona farasi na waendesha farasi wakiwa juu ya farasi. Walionekana hivi: Walivaa dirii za chuma vifuani mwao zilizokuwa za rangi nyekundu, rangi ya bahari iliyoiva na za rangi ya njano kama baruti. Vichwa vya farasi vilionekana kama vichwa vya simba. Farasi walikuwa wanatoa moto, moshi na baruti katika vinywa vyao.
18Theluthi ya watu wote duniani walikufa kutokana na mapigo haya matatu yaliyokuwa yanatoka vinywani mwa farasi: moto, moshi na baruti.
19Nguvu ya farasi ilikuwa kwenye midomo na mikia yao. Mikia yao ilikuwa kama nyoka walio na vichwa vya kuwauma na kuwadhuru watu.
20Watu wengine duniani hawakufa kwa mapigo haya. Lakini watu hawa bado hawakubadili mioyo yao na kuacha kuabudu vitu walivyovitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Hawakuacha kuabudu mapepo na sanamu zilizotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, au kusikia au kutembea.
21Hawakubadili mioyo yao na kuacha kuua watu wengine au kuacha uchawi, dhambi ya uzinzi na wizi.