Warumi 2

Warumi 2

Huwezi Kuwahukumu Wengine

1Je! unadhani unaweza kuwahukumu watu wengine? Unakosea. Wewe pia una hatia ya dhambi. Unawahukumu kwa kuwa wanatenda mabaya, lakini wewe unatenda yale wanayotenda. Hivyo unapowahukumu, unajihukumu wewe mwenyewe.

2Lakini tunajua kwamba Mungu yuko sahihi kwa kuwahukumu wote wanaotenda mambo ya jinsi hiyo!

3Lakini kwa kuwa unatenda mambo sawa na wale unaowahukumu, hakika unaelewa kuwa Mungu atakuadhibu nawe pia. Unawezaje kufikiri kuwa utaiepuka hukumu yake?

4Mungu amekuwa mwema kwako. Na amekuwa mvumilivu sana, akisubiri ubadilike. Lakini haufikirii jambo lolote kuhusu wema wake mkuu. Pengine huelewi kwamba Mungu ni mwema kwako ili ubadili moyo na maisha yako.

5Lakini wewe ni mkaidi sana! Unakataa kubadilika. Hivyo unaikuza hukumu yako wewe mwenyewe zaidi na zaidi. Utahukumiwa siku ile ambapo Mungu ataonesha hasira yake. Siku ambayo kila mtu ataona Mungu anavyowahukumu watu kwa haki.[#2:5 Tazama Rum 1:18; 2:1.]

6Kama anavyosema, “Atamlipa au kumwadhibu kila mtu kutokana na matendo yale.”[#Zab 62:12; Mit 24:12]

7Watu wengine hawachoki kutenda mema. Wanaishi kwa ajili ya utukufu na heshima kutoka kwa Mungu na kwa ajili ya maisha yasiyoweza kuharibiwa. Mungu atawapa watu hao uzima wa milele.

8Lakini wengine hutenda mambo yanayowafurahisha wao wenyewe. Hivyo hukataa yaliyo haki na huchagua kutenda mabaya. Watateseka kwa hukumu ya Mungu yenye hasira.

9Matatizo na mateso yatampata kila mmoja anayetenda uovu; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi.

10Lakini atampa utukufu, heshima na amani kila atendaye mema; wale wote wanaotenda mema; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi.

11Ndiyo, Mungu humhukumu kila mtu pasipo upendeleo, bila kujali yeye ni nani.

12Watu walio na sheria na wote ambao hawajawahi kuisikia sheria, wote wako sawa wanapotenda dhambi. Watu wasio na sheria na ni watenda dhambi wataangamizwa. Vivyo hivyo, wale walio na sheria na ni watenda dhambi watahukumiwa kuwa na hatia kwa kutumia sheria.

13Kuisikia sheria hakuwafanyi watu wawe wenye haki kwa Mungu. Wanakuwa wenye haki mbele zake, pale wanapotekeleza kile kinachoagizwa na sheria.

14Fikirini kuhusu wasio Wahayudi ambao hawakukua wakiwa na sheria. Wanapotenda kama sheria inavyoamuru, wanakuwa kielelezo cha sheria, ijapokuwa hawana sheria iliyoandikwa.[#2:14 Au “… hawana sheria. Lakini wanapotenda yale yanayoamriwa na sheria kwa kufuata utashi wa asili …”.]

15Wanaonesha kuwa wanafahamu kilicho sahihi na kibaya, kama sheria inavyoamuru na dhamiri zao zinakubali. Lakini wakati mwingine mawazo yao huwaambia kuwa wamekosea au wamefanya sahihi.

16Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu kupitia Yesu Kristo, sawasawa na Habari Njema ninayoihubiri.

Wayahudi na Sheria

17Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu.

18Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria.

19Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani.

20Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote.

21Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba.

22Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao.

23Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake.

24Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.”[#2:24 Isa 52:5. Tazama pia Eze 36:20-23.]

25Ikiwa mnaifuata sheria, basi kutahiriwa kwenu kuna maana. Lakini mkiivunja sheria, mnakuwa kama watu ambao hawakutahiriwa.

26Wale wasiokuwa Wayahudi hawatahiriwi. Lakini wakiifuata sheria inavyosema, wanakuwa kama watu waliotahiriwa.

27Mnayo sheria na tohara, lakini mnaivunja sheria. Hivyo wale wasiotahiriwa katika miili yao, lakini bado wanaitii sheria, wataonesha kuwa mna hatia.

28Wewe si Myahudi halisi ikiwa utakuwa Myahudi tu kwa nje. Tohara halisi si ile ya nje ya mwili tu.

29Myahudi halisi ni yule aliye Myahudi kwa ndani. Tohara halisi inafanywa moyoni. Ni kitu kinachofanywa na Roho, na hakifanyiki ili kufuata sheria iliyoandikwa. Na yeyote aliyetahiriwa moyoni kwa Roho hupata sifa kutoka kwa Mungu, siyo kutoka kwa watu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International