Isaya 4

Isaya 4

1Wakati huo wanawake saba watamvamia mwanamume mmoja na kumwambia, “Chakula na mavazi tutajitafutia wenyewe, lakini wewe utuondolee aibu yetu, uturuhusu tuitwe kwa jina lako.”

Mji wa Yerusalemu utarekebishwa

2Siku ile, tawi atakalochipusha Mwenyezi-Mungu litakuwa zuri na tukufu, nayo matunda ya nchi yatakuwa ya fahari na utukufu kwa wale Waisraeli watakaosalia. Waisraeli watakaobaki watayaonea fahari na kujivunia mazao ya nchi yao.

3Wale watakaosalia hai mjini Yerusalemu, naam, wale watakaobaki huko Siyoni, wataitwa “Wateule wa Mungu;” hao ndio wale wote watakaokuwa wameandikwa kitabuni mwake waishi huko Yerusalemu.

4Kwa roho yake, Bwana atawaweka sawa na kuwatakasa. Na atakapokwisha kuwatakasa wanawake wa Siyoni uchafu wao na kufuta madoa ya damu yaliyomo humo Yerusalemu,

5hapo atafanya kila mahali juu ya mlima Siyoni na juu ya mikutano ya watu kuwe na wingu wakati wa mchana, na moshi na moto uwakao vizuri wakati wa usiku. Zaidi ya hayo utukufu wa Mungu utaufunika na kuulinda mji wote.[#4:5 Taz Kut 13:21; 24:16]

6Utukufu wake utakuwa kwao kivuli kuwakinga na joto la mchana; na kimbilio na kinga yao wakati wa dhoruba na mvua.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania