Zaburi 140

Zaburi 140

Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu

1Ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe na watu wabaya,

unikinge na watu wakatili.

2Watu hao huwaza mabaya daima,

huzusha magomvi kila mara.

3Ndimi zao hatari kama za nyoka;[#Taz Rom 3:13]

midomoni mwao mna maneno ya sumu kama ya joka.

4Ee Mwenyezi-Mungu, unilinde na makucha ya wabaya;

unikinge na watu wakatili

ambao wamepanga kuniangusha.

5Wenye kiburi wamenitegea mitego,

wametandaza kamba kama wavu,

wameficha mitego njiani wanikamate.

6Namwambia Mwenyezi-Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”

Usikilize, ee Mwenyezi-Mungu, sauti ya ombi langu.

7Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu, mkombozi wangu mkuu,

umenikinga salama wakati wa vita.

8Ee Mwenyezi-Mungu, usiwape waovu wanayotaka;

wala mipango yao mibaya usiifanikishe.

9Hao wanaonizingira wanainua vichwa;

uovu wa maneno yao uwapate wao wenyewe!

10Makaa ya moto yawaangukie;

watumbukizwe mashimoni, wasiinuke tena.

11Wanaowasengenya wengine wasifanikiwe katika nchi;

uovu uwapate wakatili na kuwaangamiza mara!

12Najua Mwenyezi-Mungu hutetea kisa cha wanaoteswa,

na kuwapatia haki maskini.

13Hakika waadilifu watalisifu jina lako;

wanyofu watakaa kwako.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania