The chat will start when you send the first message.
1Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;
yeye ni msaada wetu daima wakati wa taabu.
2Kwa hiyo hatutaogopa chochote,
dunia ijapoyeyuka
na milima kutikisika kutoka baharini;
3hata kama bahari ikichafuka na kutisha,
na milima ikatetemeka kwa machafuko yake.
4Kuna mto ambao maji yake hufurahisha mji wa Mungu,
makao matakatifu ya Mungu Mkuu.
5Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;
Mungu ataupa msaada alfajiri na mapema.
6Mataifa yaghadhibika na tawala zatikisika;
Mungu anguruma nayo dunia yayeyuka.
7Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
8Njoni mwone matendo ya Mwenyezi-Mungu;
oneni maajabu aliyoyafanya duniani.
9Hukomesha vita popote duniani,
huvunjavunja pinde na mikuki,
nazo ngao huziteketeza.
10Asema: “Nyamazeni na kujua kuwa mimi ni Mungu!
Mimi natukuka katika mataifa yote;
mimi natukuzwa ulimwenguni kote!”
11Mwenyezi-Mungu wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.