Zaburi 58

Zaburi 58

Mungu hakimu wa mahakimu

1Enyi watawala, je, mwahukumu kwa haki kweli?[#58:1 au Miungu.]

Je, mnawahukumu watu kwa adili?

2La! Nyinyi mwafikiria tu kutenda maovu;

nyinyi wenyewe mwaeneza dhuluma nchini.

3Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao,

waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa.

4Wana sumu kama sumu ya nyoka;

viziwi kama joka lizibalo masikio,

5ambalo halisikii hata sauti ya mlozi,

au utenzi wa mganga stadi wa uchawi.

6Ee Mungu, wavunje meno yao,

yangoe, ee Mwenyezi-Mungu, meno ya simba hao.

7Watoweke kama maji yanayodidimia mchangani,

kama nyasi wakanyagwe na kunyauka,

8watoweke kama konokono ayeyukavyo,

kama mimba iliyoharibika isiyoona kamwe jua!

9Kabla hawajatambua, wangolewe

kama miiba, michongoma au magugu.

Kwa hasira ya Mungu, wapeperushwe mbali,

wakiwa bado hai.

10Waadilifu watafurahi waonapo waovu wanaadhibiwa;

watatembea katika damu ya watu wabaya.

11Watu wote watasema: “Naam, waadilifu hupata tuzo!

Hakika yuko Mungu anayeihukumu dunia!”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania