The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;[#Taz Zab 38:1]
usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu;
uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani.
3Ninahangaika sana rohoni mwangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini?
4Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe;
unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako.
5Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka;
huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu?
6Niko hoi kwa kilio cha uchungu;
kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi;
kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu.
7Macho yangu yamechoka kwa huzuni;
yamefifia kwa kutaabishwa na adui.
8Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu![#Taz Mat 7:23; Luka 13:27]
Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu.
9Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu;
Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu.
10Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika;
watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla.