The chat will start when you send the first message.
1Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako.[#5:1 Yaani, sisi ni watu wa ukoo na kabila lako. Kwa namna moja au nyingine, watu wa Israeli walikuwa na uhusiano wa jamaa. Msemo wenyewe una shabaha ya kutilia mkazo jambo hilo. Rejea Mwa 2:23; Amu 9:2-3.]
2Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’”[#5:2 Ahadi ya Mwenyezi-Mungu kwa Daudi inarudiwa hapa na pale kwa maneno mbalimbali katika vitabu vya Samueli (1Sam 13:13-14; 25:30; 2Sam 3:9,18; 7:17-29).]
3Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli.
4Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini.[#5:4 Hapa, kama vile katika mahali pengine katika Biblia, idadi hizo ni idadi za jumla na hazipaswi kuchukuliwa kama idadi kamili.]
5Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.
6Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo.[#5:6 Wayebusi waliishi nchini Kanaani muda mrefu kabla ya Waisraeli kuinyakua nchi hiyo. Yerusalemu mmojawapo ya miji yao ulikuwa mpakani mwa makabila ya Yuda na Benyamini.]
7Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.
8Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.”[#5:8 Huu ulikuwa mfereji wa chini kwa chini ambao ulikuwa umepita chini ya ukuta wa Yerusalemu kutoka chemchemi za Gihoni nje ya mji na kuingia katika bwawa lililokuwa ndani ya mji.; #5:8 Makala ya Kiebrania si dhahiri. Wengine wanafikiri Daudi anarudia maneno yale yale “vilema na vipofu” ambayo walisema Wayebusi (aya 6) ili kuwakebehi wao wenyewe.]
9Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo kuelekea ndani.[#5:9 Labda jina hilo linataja sehemu ambayo ilitegemeza matuta yaliyotegemeza mteremko wa upande wa mashariki wa mji huo.]
10Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.[#5:10 Taz 1Sam 1:3 maelezo na pia “Orodha ya Majina ya Mungu” katika Kut 3:14.]
11Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu.[#5:11 Tiro ulikuwa bandari maarufu ya Foinike katika pwani ya Bahari ya Mediteranea. Daudi na baadaye Solomoni walifanya mikataba na Hiramu awapatie vifaa na mafundi wajenzi (1Fal 5:12—18:1; 1 Nya 14:1; 2Nya 2:3-12).]
12Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli.
13Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike.[#5:13 Taz 3:7 maelezo.]
14Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni,
15Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia,
16Elishama, Eliada na Elifeleti.
17Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome.
18Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu.
19Basi, Daudi alimwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Daudi, “Nenda, maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
20Basi, Daudi akafika Baal-perasimu, na kuwashinda Wafilisti; halafu akasema, “Mwenyezi-Mungu amepita katikati ya adui zangu kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-perasimu.[#5:20 Kiebrania maana yake “Bwana apitaye katikati”.]
21Wafilisti waliziacha sanamu zao za miungu mahali hapo, naye Daudi na watu wake wakazichukua.[#5:21 Ilikuwa kawaida wakati wa vita kwa watu wa nyakati za kale kubeba sanamu za miungu yao. Waisraeli nao pia walibeba sanduku la agano walipokwenda kupigana na Wafilisti (taz 1Sam 4:1-7).]
22Kwa mara ya pili, Wafilisti walifika tena na kujitawanya kwenye bonde la Refaimu.
23Daudi alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa ulipo, bali zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala wa miti na miforosadi.
24Na mara mtakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya miforosadi hiyo, hapo jipe moyo kwani nitakuwa nimetoka ili kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.”
25Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, naye akawapiga Wafilisti kutoka Geba hadi Gezeri.