The chat will start when you send the first message.
1“Kwa hiyo, Bwana ametekeleza sasa jambo lile alilotamka dhidi yetu, na dhidi ya mahakimu wetu wanaoongoza Israeli, dhidi ya wafalme wetu, wakuu wetu na watu wa Israeli na Yuda.
2Hapana mahali popote pengine duniani palipopata kutukia mambo yaliyotukia huko Yerusalemu, Bwana alipotekeleza yale yaliyoandikwa katika sheria ya Mose.
3Mambo yalikuwa mabaya kiasi cha mtu kumla mwanawe na mwingine kumla bintiye![#2:3 Tukio la aina hiyo linatajwa katika Lawi 26:29; Kumb 28:53; 2Fal 6:24-31; Yer 19:9; Omb 2:20; 4:10 kama mambo ya kuchukiza yanayotokana na vita.]
4Bwana alitutia mikononi mwa tawala zote zilizotuzunguka tukadharauliwa na kuaibishwa kati ya mataifa yote ambako alitutawanya.
5Kwa vile tulitenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wetu kwa kutokutii sauti yake, basi, taifa letu likashindwa badala ya kuwa mshindi.
6“Bwana Mungu wetu ni mwadilifu lakini sisi kama tulivyo leo tumejaa aibu kama vile wazee wetu!
7Maafa yote aliyotutishia nayo Bwana wetu yametupata.
8Hata hivyo hatukumgeukia na kuomba ili kila mmoja wetu aachane na mawazo ya moyo wake mwovu.
9Basi, Bwana ameona ni lazima ayalete yale maafa aliyosema, nayo yametupata; maana Bwana ni mwadilifu kuhusu yote yale aliyotuagiza tuyafanye.[#2:9 Dan 9:14; taz Bar 2:20,24. Tafsiri nyingine yamkini: “Bwana ameyasimamia yale maafa yafike kama alivyosema”; rejea pia Yer 1:12.]
10Lakini sisi hatukutii sauti yake aliposema tuishi kufuatana na amri zake alizotupa.
11“Sasa, ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa mkono wako wenye nguvu, kwa miujiza, kwa nguvu kuu na kwa mkono wako ulionyoshwa, ukalipatia sifa jina lako hadi leo.
12Tumetenda dhambi; tumekuwa waovu, tumekosa, ee Bwana Mungu wetu, tukazivunja amri zako zote.[#2:12 Taz 1Fal 8:47 ambapo vitenzi vitatu vya maana karibu hiyo hiyo vinatumiwa, tena katika mazingira ya uhamishoni; rejea pia Zab 106:6.]
13Lakini tunakuomba usiendelee kutukasirikia maana humu ulimotutawanya kati ya mataifa mengine tumeachwa na wachache.[#2:13 Kumb 4:27; Isa 1:9; 4:3; Yer 42:2.]
14Usikilize ee Bwana, sala yetu na ombi letu; utuokoe, kwa hisani yako, utujalie tupendeke mbele ya hao waliotupeleka uhamishoni.[#2:14 Yamkini si vitu viwili ila ni namna ya kusema wazo moja kwa maneno mawili na maana yake ni “sala ya moyo”. Rejea Dan 9:17.]
15Hapo dunia yote itatambua kwamba wewe ndiwe Bwana Mungu wetu na kwamba wewe umelichagua taifa la Israeli kuwa watu wako mwenyewe.
16Ee Bwana, utuangalie hapa chini kwa wema, kutoka makao yako matakatifu. Utege sikio lako ee Bwana, utusikilize.
17Ufumbue macho yako, ututazame. Wafu walio kuzimu ambao hawana pumzi tena mwilini mwao hawawezi kukutukuza na kutangaza ulivyo mwadilifu wewe Bwana.[#2:17 Zab 6:6. Picha tunayopewa hapa kuhusu wafu na makao ya wafu ni ya kawaida katika A.K.; rejea Zab 30:9; 88:10-12; Mhub 9:5-6; Sira 17:28.]
18Lakini watu walio hai, wamelegea, wanyonge, vipofu na wenye njaa ndio hao wanaoweza kukutukuza ee Bwana na kutangaza uadilifu wako.
19“Ee Bwana, Mungu wetu, maombi yetu hatuyaleti mbele yako tukitegemea matendo yoyote mema ya wazee wetu au ya wafalme wetu.[#2:19 Au, “Mastahili ya wazee wetu”. Taz Dan 9:18; Gal 2:16; Tito 3:5.]
20Wewe umeielekeza ghadhabu na hasira yako dhidi yetu kama ulivyoonya hapo awali kwa njia ya watumishi wako manabii waliposema:
21‘Bwana asema hivi: Inamisheni mabega yenu mkamtumikie mfalme wa Babuloni nanyi mtaweza kukaa katika nchi niliyowapa wazee wenu.[#2:21 Yer 27:11-12. Kuinamisha mabega ni picha ya utii au kunyenyekea.]
22Lakini msipotii sauti ya Bwana, mkakataa kumtumikia mfalme wa Babuloni,
23basi, nitakomesha ishara yoyote ya furaha na sherehe katika miji ya Yuda na Yerusalemu. Hapatakuwa na sauti za sherehe za harusi. Nchi yote itaachwa ukiwa na mahame!’[#2:23 Au, “sauti … ya furaha”; Yer 7:34; 16:9; 25:10.]
24“Lakini sisi hatukutii sauti yako juu ya kumtumikia mfalme wa Babuloni, nawe umetekeleza yale uliyosema kwa njia ya watumishi wako manabii, uliposema kwamba mifupa ya wafalme wetu na ya wazee wetu itafukuliwa makaburini.[#2:24 Taz Yer 8:1-2.]
25Na, kwa kweli imetupwa kwenye joto la mchana na baridi kali usiku. Wao walikufa katika mateso ya njaa, vita na maradhi mabaya.
26Tena umeifanya nyumba ile ambamo sisi tulikuabudu kuwa uharibifu mtupu kama ilivyo leo hii, kwa sababu ya maovu ya watu wa Israeli na watu wa Yuda.
27“Hata hivyo, ee Bwana, wewe umetuvumilia kwa wema na huruma yako kuu,
28sawa kabisa na yale uliyotangaza kwa njia ya Mose mtumishi wako, siku ile ulipomwamuru aiandike sheria yako mbele ya Waisraeli, ukisema,
29‘Kama hamtatii sauti yangu, basi, nyinyi mlio jumuiya kubwa mtabaki wachache tu kati ya mataifa ambamo mimi nitawatawanyeni.
30Najua kwamba hamtanitii maana nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu. Lakini mtakapokuwa uhamishoni ndipo mtapata akili,
31na kutambua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu. Mimi nitawapeni moyo wa utii na masikio masikivu.
32Mtanitukuza na kunikumbuka katika nchi hiyo mtakayohamishiwa.
33Mtaachana na ukaidi wenu na matendo yenu maovu, maana mtakumbuka yaliyowapata wazee wenu wakati walipotenda dhambi mbele ya Bwana.
34Kisha nitawarudisheni katika nchi ile niliyoapa kuwapa wazee wenu, ahadi niliyompa Abrahamu, Isaka na Yakobo, nanyi mtaimiliki. Nami nitawafanyeni muwe wengi wala hamtapungua tena.
35Nitafanya nanyi agano la milele niwe Mungu wenu, nanyi muwe watu wangu. Nami sitawaondoeni tena, nyinyi watu wangu wa Israeli kutoka katika nchi hiyo niliyowapeni.’[#2:35 Hili agano la milele (sawa na agano linalotajwa katika Yer 31:31-34), halitahusu tu jambo la kupata fanaka za nyakati zilizopita, ila Mungu mwenyewe atalitekeleza hilo kwa namna mpya kabisa. Rejea pia Yer 32:38-40; Eze 36—37; Amo 9:15.]