The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo, manabii wawili, Hagai na Zekaria, mwana wa Ido, waliwatolea unabii Wayahudi waliokuwa wanakaa Yuda na Yerusalemu, katika jina la Mungu wa Israeli.
2Nao Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yeshua, mwana wa Yosadaki, walipousikia ujumbe huo walianza tena kuijenga nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, wakisaidiwa na manabii wa Mungu.
3Baadaye Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, walikwenda Yerusalemu na kuuliza, “Nani aliyewaamuru kuijenga nyumba hii mpaka kuimaliza?”[#5:1-3 Simulizi kuhusu jinsi Hagai na Zekaria walivyowahimiza watu kukamilisha ujenzi wa hekalu limo katika kitabu cha Hagai na sura nane za kwanza za Zekaria. Maandishi ya kumbukumbu ya Babuloni ya mwaka 502 K.K. inamtaja “Tatenai” kuwa gavana wa Mkoa wa Magharibi. Taz tena 4:8-10.]
4Pia waliuliza, “Ni akina nani wanaojenga nyumba hii? Tunataka majina yao.”
5Lakini Mungu alikuwa anawalinda viongozi wa Wayahudi, kwa hiyo maofisa hao hawakuwakataza mpaka hapo walipomwandikia mfalme Dario na kupata maoni yake.
6Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na wenzao, wakamwandikia mfalme Dario.
7Ifuatayo ni ripoti waliyompelekea mfalme:
“Kwa mfalme Dario; tunakutakia amani.
8Tungetaka kukufahamisha ee mfalme, kuwa tulikwenda mkoani Yuda ilipo nyumba ya Mungu Mkuu. Nyumba hii inajengwa upya kwa mawe makubwamakubwa na kuta zake zinawekwa boriti za miti. Kazi hiyo inafanywa kwa uangalifu mkubwa na inaendelea vizuri sana.
9Tuliwauliza viongozi hao watuambie ni nani aliyewapa amri ya kuijenga upya nyumba hii mpaka kuimaliza.
10Tuliwauliza pia majina yao ili tuweze kukujulisha wale wanaoongoza kazi hiyo.
11“Wao walitujibu hivi: ‘Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na dunia, na tunaijenga upya nyumba ambayo ilikuwa imejengwa na kumalizika hapo awali na mfalme mmoja mkuu wa Israeli.[#5:11 Hili ni jina la sifa la Mungu ambalo ni kamili zaidi kuliko lile la “Mungu wa mbingu” (1:2).; #5:11 Hapa yamkini yahusu mfalme Solomoni ambaye alitawala yapata mwaka 970 mpaka 931 K.K. na ambaye ndiye aliyejenga hekalu la kwanza (1Fal 6:37-38).]
12Lakini kwa kuwa babu zetu walimkasirisha Mungu wa mbingu, yeye aliwatia mikononi mwa mfalme Nebukadneza wa Babuloni, Mkaldayo, aliyeiharibu nyumba hii na kuwapeleka watu uhamishoni huko Babuloni.[#5:12 Maneno “kutia mikononi mwa …” mara nyingi yanamaanisha “kuweka katika mateso” (hapa kwa maana ya kuwaadhibu kwa sababu walivunja agano lake). Neno “Mkaldayo” linamtaja Nebukadneza kama mmoja wa Wakaldayo ambao walikuwa wakazi wa Kusini mwa Mesopotamia na pengine ni sawa na Wababuloni. Nebukadneza alianzisha himaya mpya ya Babuloni wakati utawala wa Ashuru ulipoangushwa katika mwaka 612 K.K. na utawala huo mpya uliendelea mpaka ulipoangushwa na Wapersi mwaka 539 K.K.]
13Lakini mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake mfalme Koreshi wa Babuloni alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya.
14Pia alivirudisha vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka katika hekalu huko Yerusalemu na kuviweka katika hekalu la Babuloni. Vyombo hivyo Koreshi aliviondoa hekaluni Babuloni na kumkabidhi Sheshbaza ambaye alikuwa amemteua awe mtawala wa Yuda; alimwamuru[#5:14 Taz 1:8 maelezo.]
15achukue vyombo hivyo na kuvirudisha katika hekalu la Yerusalemu, na kuijenga upya nyumba ya Mungu mahali pake.
16Kisha Sheshbaza alikuja na kuweka msingi wa nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu, na tangu wakati huo ujenzi umekuwa ukiendelea mpaka sasa, lakini bado haijamalizika.’
17Basi, ukipenda ewe mfalme, amuru uchunguzi ufanywe katika kumbukumbu za kifalme mjini Babuloni kama mfalme Koreshi alitoa amri nyumba hii ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu. Kisha, tunakuomba utujulishe maoni yako kuhusu jambo hili.”