Wagalatia 2

Wagalatia 2

Paulo na mitume wengine

1Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami.[#2:1 Yaani baada ya kukaa kule Kilikia (Gal 1:21); au, tangu tukio la njiani kwenda Damasko (Gal 1:15-16).; #2:1 Mwenzake Paulo katika miaka ya mwanzoni ya safari zake za kuhubiri (Mate 4:36; 13:1—15:39).; #2:1 Mwenzake na msaidizi wake Paulo (2Kor 7:6; 8:6,16-17; Tito 1:4).]

2Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Injili niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa, isije ikawa bure.

3Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa,

4ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa.[#2:4 Rejea Mate 15:1,24.; #2:4 Wazo hili la uhuru ni la kiwango cha juu kabisa katika barua hii. Uhuru wa Kikristo ni kinyume cha kuwa chini ya utumwa wa sheria ya Mose (Gal 5:1,13).]

5Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima.

6Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi — kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje — watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea.

7Badala yake, walitambua kwamba Mungu alikuwa amenituma kuhubiri Injili kwa watu wa mataifa mengine kama vile Petro alivyokuwa ametumwa kuihubiri kwa Wayahudi.

8Maana, yule aliyemwezesha Petro kuwa mtume kwa Wayahudi, ndiye aliyeniwezesha nami pia kuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine.

9Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, ambao waonekana kuwa viongozi wakuu, walitambua kwamba Mungu alinijalia neema hiyo, wakatushika sisi mkono, yaani Barnaba na mimi, iwe ishara ya ushirikiano. Sisi ilitupasa tukafanye kazi kati ya watu wa mataifa mengine, na wao kati ya Wayahudi.[#2:9 Yakobo (taz Gal 1:19 maelezo), Kefa (taz Gal 1:18 maelezo) na Yohane (mtume), wote hawa watatu walijulikana kama “viongozi maarufu” (neno kwa neno: nguzo) katika Kanisa la Yerusalemu.]

10Wakatuomba lakini kitu kimoja: tuwakumbuke maskini; jambo ambalo nimekuwa nikijitahidi kutekeleza.[#2:10 Rejea Mate 11:29-30. Wakati fulanifulani Paulo alijitolea kukusanya mchango wa msaada kwa ajili ya maskini wa kanisa la Yerusalemu (rejea Rom 15:25-26; 1Kor 16:1-4; 2Kor 8:1-4).]

Paulo anamkaripia Petro

11Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea.[#2:11 Yaani, Antiokia katika Siria (Mate 11:19-26). Huu ulikuwa mji wa tatu kwa ukubwa katika dola la Waroma.]

12Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara.[#2:12 Yaani, Wakristo wasio Wayahudi. Kula pamoja nao ilikuwa kinyume cha sheria na desturi za Kiyahudi (rejea Mate 10:1-48; 11:1-3,17-18). Petro alipoacha baadaye kula na Wakristo wasio Wayahudi ilikuwa ishara kwamba hakuwapokea kama ndugu wenye haki kamili katika Kanisa la Kikristo.]

13Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao.

14Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Injili haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?”

Wayahudi na watu wa mataifa mengine huokolewa kwa imani

15Kweli, sisi kwa asili ni Wayahudi, na si watu wa mataifa mengine wenye dhambi![#2:15 Wayahudi walikuwa na desturi ya kuwaita watu wa mataifa mengine “wenye dhambi” kwa vile waliwaona kuwa wako nje ya kundi la watu walioteuliwa na Mungu.]

16Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kufanywa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii sheria.[#2:16 Taz pia Zab 143:2 ambapo tunaambiwa kuwa hakuna mtu aliye mwadilifu mbele ya Mungu. Zaburi hiyo inanukuliwa pia katika Rom 3:20.; #2:16 Taz Rom 1:17 maelezo na rejea pia Gal 3:24. Wazo la kufanywa waadilifu kwa kumwamini Yesu Kristo na sio kwa kutegemea sheria linazungumziwa kwa kina zaidi katika Rom 3:19—4:5; rejea pia Mate 15:10-11; Efe 2:8-9.]

17Sasa, ikiwa katika kutafuta tufanywe waadilifu kwa kuungana na Kristo sisi tunaonekana kuwa wenye dhambi, je, jambo hili lina maana kwamba Kristo anasaidia utendaji wa dhambi? Hata kidogo!

18Lakini ikiwa ninajenga tena kile nilichokwisha bomoa, basi nahakikisha kwamba mimi ni mhalifu.[#2:18 Yaani, sheria kama chombo kiwezacho kuleta wokovu. Maneno haya yanaelezwa katika 1:19-20.]

19Maana, kuhusu sheria hiyo, mimi nimekufa; sheria yenyewe iliniua, nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani,[#2:19 Si rahisi kufuata na kuelewa hoja ya Paulo hapa. Ni lazima kwanza kufuata anayosema katika sehemu ya pili ya aya hii: “Mimi nimesulubiwa pamoja na Kristo”. Mkristo amekufa pamoja na Kristo kuhusu dhambi na kuhusu sheria, ili aishi uhai mpya (rejea Rom 6:3-11; 7:4-5). Inawezekana pia kusema kwamba kifo hicho kilifanyika kwa njia ya sheria, kwa vile Yesu alihukumiwa kuuawa kufuatana na sheria (rejea Yoh 19:7; Gal 3:13).; #2:19-20 Kinachosemwa hapa ni jambo la msingi katika imani ya Kikristo (Gal 5:24; 6:14; rejea Rom 6:1-14; 8:10-11; Fil 1:21). Ingawa kwa ulimwengu msalaba ulikuwa ishara ya kifo, kwa Paulo na kwa wote wanaomwamini Kristo ni uhai mpya. Kifo cha Kristo kiliwapa watu uhuru na kuwaondoa kutoka laana ya sheria.]

20na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.

21Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu hufanywa mwadilifu kwa njia ya sheria, basi, Kristo alikufa bure!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania