The chat will start when you send the first message.
1Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye kuhani mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mkuu mbinguni.[#8:1 Katika Ebr 8:1—10:18 wadhifa wa Yesu kama kuhani mkuu halisi au wa kweli unaelezwa kwa uangalifu. Taz Ebr 2:17 maelezo.]
2Yeye hutoa huduma ya kuhani mkuu mahali patakatifu katika maskani, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu.[#8:2 Kwa kutofautisha na ile hema ya mkutano waliyojifanyia Waisraeli kule jangwani (rejea Kut 26) na ambayo mwandishi anaiona kuwa mfano tu wa ile ya kweli (taz 8:3-5 maelezo).; #8:1-2 Rejea Zab 110:1. Mawazo mawili: “mfalme” (upande wa kulia wa Mungu Mkuu) na “kuhani” (aya 2; Zab 110:4) inatumiwa hapa juu ya Yesu. Taz Ebr 1:13 maelezo, na 2:17 maelezo.]
3Kila kuhani mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu zawadi na tambiko, na hivyo kuhani mkuu wetu lazima naye awe na kitu cha kutolea.[#8:3 Taz Ebr 7:27 maelezo, rejea Ebr 10:10.]
4Kama yeye angekuwa wa hapa duniani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na sheria.
5Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Maana Mose alipokuwa karibu kuitengeneza ile maskani, Mungu alimwambia: “Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano uliooneshwa kule mlimani.”[#8:3-5 Rejea Ebr 9:11,23-24; 10:1. Rejea pia Kut 25:40. Yesu Kristo na ile hema ya kweli (aya 2) ni kweli zisizoonekana kwa macho, kweli ambazo kuhani wa Wayahudi na hema ya A.K. vilikuwa vielelezo tu vya kweli hizo; kwa kifupi, Agano Jipya (aya 7) ni ukweli ambao ulitanguliwa kuelezwa kwa mfano tu katika A.K.]
6Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.[#8:6 Au, “Amekuwa mpatanishi bora zaidi kati ya Mungu na watu”: Ebr 9:15; 12:24; taz 1Tim 2:5. Ukuu wa Yesu Kristo unatiliwa mkazo.]
7Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.[#8:7 Mkataba aliouweka Mungu pamoja na Waisraeli Mlimani Sinai (aya 9; rejea Kut 19—20; 24:3-8).]
8Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema:
“Siku zinakuja, asema Bwana,
ambapo nitafanya agano jipya
na watu wa Israeli na wa Yuda.
9Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao
siku nilipowaongoza kwa mkono kutoka Misri.
Hawakuwa waaminifu kwa agano langu;
na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
10Hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana:
Nitaweka sheria zangu akilini mwao,
na kuziandika mioyoni mwao.
Mimi nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11Hakuna atakayemfundisha mwananchi mwenzake,
wala atakayemwambia ndugu yake:
‘Mjue Bwana’.
Maana wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
12Nitawasamehe makosa yao,
wala sitakumbuka tena dhambi zao.”
13Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.