The chat will start when you send the first message.
1Yafuatayo ni maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani wa mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini.[#1:1 Msemo huu unatafsiri neno la Kiebrania ambalo katika mazingira mbalimbali ya maandishi lahusu “matukio” au “mikasa”, au “ujumbe”. Kitabu cha Yeremia sio tu kwamba kina maneno ya nabii ila pia masimulizi mengi yaliyomsibu katika huduma yake kama nabii wa Mungu. Na kuhusu “Hilkia”, baba yake Yeremia, si sawa na kuhani Hilkia ambaye aligundua kitabu cha sheria hekaluni (2Fal 22:8). Na kuhusu “Anathothi” tunajua kwamba ulikuwa mahali kilomita 5 kaskazini-mashariki ya Yerusalemu na unatajwa kama mojawapo ya miji ya “kukimbilia usalama” ya Walawi (Yos 21:13-18). “Benyamini” alikuwa mtoto wa mwisho wa Yakobo na Raheli (Mwa 35:16-18). Kabila la Yuda na Benyamini yalikuwa makabila mawili pekee yaliyofanya utawala wa kusini wa Yuda.; #1:1-3 Kuhusu aya hizi za kwanza ambazo zinatumika kama utangulizi wa kitabu hiki, Taz Isa 1:1 maelezo.]
2Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda.[#1:2 Yosia alitawala mnamo mwaka 640-609 K.K.; kwa hiyo mwaka wa 13 wa utawala wake, wakati Yeremia alipoitwa kuwa nabii, ulikuwa mwaka 627. Rejea 2Fal 22:1-23:30; 2Nya 34—35.]
3Lilimjia tena wakati Yehoyakimu mwana wa Yosia, alipokuwa mfalme wa Yuda. Yeremia aliendelea kupata neno la Mwenyezi-Mungu hadi mwishoni mwa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Mnamo mwezi wa tano wa mwaka huo, watu wa Yerusalemu walipelekwa uhamishoni.[#1:3 Rejea 2Fal 23:36-25:7 na pia taz Yer 22:30 maelezo.; #1:3 Uhamisho huu wa wakazi wa Yuda hadi Babuloni ulifanyika mwaka 586 K.K. (rejea 2Fal 25:8-21). Yeremia hakuwa mmoja wa wahamishwa (rejea Yer 40:1-6) bali, baada ya kuangamizwa mji wa Yerusalemu, alifuatia tukio hilo na ujumbe muhimu kwa waliobaki ambao hawakupelekwa uhamishoni. Kuhusu huduma yake wakati huo rejea Yer 42—44.]
4Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake:
5“Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua,[#1:5 Yobu 10:8-12; Zab 139:13-16; rejea Yer 18:6. Kwa kusema hivyo ina maana kwamba Mwenyezi-Mungu alimjalia Yeremia uhai kwa madhumuni thabiti ya kuwa msemaji wake, yaani nabii. “Nilikujua”: Kwa maana ya Kibiblia ya “kujua” ambayo karibu kila mara katika mazingira ya namna hii yahusu uhusiano wa ndani zaidi (rejea Yoh 10:3-4,14-15) na katika mazingira mengine ya maandishi kama hapa inajumuisha utambuzi na uteuzi. Taz Amo 3:2 maelezo. “Nilikuweka wakfu”: Tafsiri ya neno la Kiebrania lenye maana ya “kutenga” kwa ajili jukumu maalumu. Rejea Isa 49:1,5. “Nabii kwa mataifa”: Nabii Yeremia anaitwa kuwa nabii sio tu kwa taifa la Waisraeli bali pia mataifa mengine (rejea Yer 25:15-58; 27; 46—51 na pia Eze 25—32).]
kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu;
nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.”
6Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu,
mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana.
7Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia,
“Usiseme kwamba wewe ni kijana bado.
Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao,
na yote nitakayokuamuru utayasema.
8Wewe usiwaogope watu hao,
kwa maana niko pamoja nawe kukulinda.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
9Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia,
“Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako.
10Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme,
uwe na mamlaka ya kung'oa na kubomoa,
mamlaka ya kuharibu na kuangamiza,
mamlaka ya kujenga na ya kupanda.”
11Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi unaochanua.”[#1:11-12 Mmea wa mlozi ni mmea wa kwanza kabisa unaochanua kabla ya mvua kubwa ya mwaka, na Kiebrania unaitwa “shaked” yaani “unachungulia” au “unakesha” au “u macho” kungojea kitu. Vivyo hivyo, Mwenyezi-Mungu anakesha au yu macho (aya 12) ili neno lake likamimilike. Rejea Isa 55:10-11; Eze 12:28.]
12Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.”
13Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.”[#1:13 Yaani kuelekea Yerusalemu na Yuda. Kaskazini ni mahali atakapotokea adui wa kuwaadhibu Waisraeli.]
14Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii.[#1:14-15 Yer 4:6; 6:1; 13:20. Haisemwi dhahiri ni nani huyo adui kutoka kaskazini ambaye atasababisha maangamizi, lakini yaonekana inahusu utawala mpya wa Babuloni. Utawala huo, hasa chini ya mfalme Nebukadneza, ulikuwa na nguvu kubwa huko Mashariki ya Kati tangu mwishoni mwa karne ya saba hadi mwanzoni mwa karne ya 6 K.K. Rejea Yer 27:6-11.]
15Maana naziita falme zote za kaskazini na makabila yote. Wafalme wake wote watakuja na kila mmoja wao ataweka kiti chake cha enzi mbele ya malango ya Yerusalemu na kandokando ya kuta zake zote, na kuizunguka miji yote ya Yuda.
16Nami nitawahukumu Waisraeli kwa ajili ya uovu wao wote wa kuniacha mimi, wakafukizia ubani miungu mingine na kuabudu sanamu walizojitengenezea wenyewe.
17Sasa basi, wewe Yeremia jiweke tayari. Haya! Nenda ukawaambie mambo yote ninayokuamuru. Usiwaogope, nisije nikakufanya mwoga mbele yao.
18Leo hii nakufanya kuwa imara kama mji uliozungukwa na ngome, kama mnara wa chuma na kama ukuta wa shaba nyeusi, dhidi ya nchi yote, dhidi ya wafalme wa Yuda, wakuu wake, makuhani wake na watu wake wote.[#1:18 Yer 15:20.]
19Watapigana nawe, lakini hawatashinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”