Yobu 42

Yobu 42

1Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu:[#42:1-6 Ingawa Yobu hakuambiwa kwa nini Mungu amemtendea hivyo, hapa katika maneno yake ya mwisho, anaonesha hali yake ya unyenyekevu na kukiri ukuu wake Mungu na mipango yake isiyochunguzika na binadamu.]

2“Najua kwamba waweza kila kitu,

lolote unalokusudia haliwezi kuzuiliwa.

3Ulisema kuwa nilithubutu kutatiza mpango wako kijinga.

Kweli nilitamka kitu ambacho sikuelewa

mambo ya ajabu mno kwangu

ambayo sikuwa ninayajua.

4Uliniambia nisikilize nawe utaniambia;[#42:4 Taz Yobu 38:3]

kwamba utaniuliza nami nikujibu.

5Kweli nilikuwa nimesikia habari zako kwa masikio tu,

lakini sasa nakuona kwa macho yangu mwenyewe.

6Kwa hiyo natubu pamoja na kujipaka mavumbi na majivu,[#42:6 Labda neno “natubu” hapa, ambalo kwa kawaida latumika kuhusu kusikitika na kuacha dhambi, linatumika kwa maana kwamba maneno yale aliyoyasema sasa anayaondoa au anayabatilisha.]

najiona mimi mwenyewe kuwa si kitu kabisa.”

Hatima

7Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Yobu, alimwambia Elifazi, Mtemani, “Ghadhabu yangu imewaka dhidi yako na marafiki zako wawili kwani hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya.[#42:7 Rejea Kumb 34:5; Yos 24:29; Isa 41:9; 42:1.]

8Kwa hiyo chukueni mafahali saba na kondoo madume saba, mwende kwa mtumishi wangu Yobu, mkawatoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yenu. Naye mtumishi wangu Yobu atawaombeeni, nami nitaisikiliza sala yake na kuacha kuwatenda kulingana na upumbavu wenu; maana hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya.”[#42:8 Yob 1:5.]

9Basi, Elifazi Mtemani, Bildadi, Mshua na Sofari Mnaamathi, wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaambia. Mwenyezi-Mungu akaipokea sala ya Yobu.

10Baada ya Yobu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi-Mungu akamrudishia Yobu hali yake ya kwanza. Alimpa maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali.

11Kisha ndugu zake, dada zake na rafiki wote waliomfahamu hapo awali wakamwendea nyumbani kwake, wakala chakula pamoja naye. Wakampa pole na kumfariji kwa ajili ya mateso yote ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemletea. Kila mmoja wao akampa Yobu fedha na pete ya dhahabu.

12Katika miaka ya Yobu iliyofuata Mwenyezi-Mungu alimbariki zaidi kuliko hata alivyokuwa amembariki pale awali. Basi Yobu akawa na kondoo 14,000, ngamia 6,000, ng'ombe 2,000 na punda majike 1,000.

13Alikuwa pia na watoto wa kiume saba na wa kike watatu.

14Binti yake wa kwanza alimpa jina Yemima, wa pili Kezia, na wa mwisho Keren-hapuki.[#42:14 Taz Yobu 1:2. Majina ya hao mabinti wa Yobu yanagusia uzuri wao: “Yemima” (njiwa), “Kezia” (mdalasini) na “Keren-hapuki” (upembe wa kuwekea mafuta). Mwandishi hataji majina ya watoto wa kiume.]

15Katika nchi yote hiyo hapakuwa na wanawake waliokuwa wazuri kama mabinti wa Yobu. Baba yao akawaachia urithi kama alivyowaachia kaka zao.[#42:15 Haikuwa kawaida kwa Wayahudi kuwaachia wasichana urithi. Taz Hes 26:33. Tukio hilo laonesha hadhi waliyopewa akina mama katika kitabu hiki cha Yobu.]

16Baada ya hapo, Yobu aliishi miaka 140, akawaona wajukuu na vitukuu vyake vyote hadi kizazi cha nne.

17Basi, Yobu akafariki akiwa mzee wa miaka mingi.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania