Yoshua 1

Yoshua 1

Mungu anamwamuru Yoshua kuiteka nchi ya Kanaani

1Baada ya kifo cha Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mose:[#1:1 Kutaja kifo cha Mose hapa hapa mwanzoni mwa kitabu hiki ni kuonesha kwamba kitabu cha Yoshua kinahusiana na Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria na habari zake zinaendelea pale Kitabu cha Kumbukumbu la Sheria kilipoachia (sura 34). Kulingana na Hes 27:18; Kumb 1:38 Mwenyezi-Mungu alikwisha mchagua Yoshua ashike nafasi ya Mose. Kabla ya kufa kwake Mose, aliweka mikono yake juu ya Yoshua kuonesha kwamba angechukua jukumu lake la kuwaongoza watu wa Mungu. Naye Mwenyezi Mungu hapa anamwamuru Yoshua awaongoze Waisraeli kwenda nchini Kanaani.; #1:1 Hapa inawezekana kutafsiri “mtumishi” kama “msaidizi” (Hes 11:28).]

2“Mtumishi wangu Mose amefariki, sasa vukeni mto Yordani, wewe pamoja na Waisraeli wote hadi kwenye nchi ile ambayo ninawapa.

3Kila mahali mtakapokanyaga nimewapeni kama nilivyomwahidi Mose.

4Mipaka ya nchi yenu itakuwa hivi: kusini ni jangwa, kaskazini ni milima ya Lebanoni, mashariki ni mto ule mkubwa Eufrate, kupitia nchi yote ya Wahiti hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi.[#1:4 Eneo la milima linalotajwa hapa liko kaskazini-mashariki ya Palestina.]

5Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe.

6Uwe imara na hodari kwa kuwa wewe utawaongoza watu hawa kuirithi nchi ambayo niliwaahidi wazee wao kuwa nitawapa.[#1:6 Ahadi hiyo ilifanyika kwa mara ya kwanza kwa Abrahamu (Mwa 17:7-8). Lakini ahadi hiyo ilikuwa na masharti yake: kutii sheria (aya 7).]

7Ila tu, uwe imara na hodari; uwe mwangalifu na kuzingatia sheria yote aliyokuamuru mtumishi wangu Mose. Fuata kila sehemu ya sheria hiyo nawe utafanikiwa popote uendapo.

8Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo.

9Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”

Yoshua anawatayarisha watu kuvuka mto Yordani

10Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu,

11“Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.”

12Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase:[#1:12-13 Baadaye, hao watakuwa na eneo lao katika mashariki ya mto Yordani. Mose alikuwa ameahidi kuwapa eneo hilo (Hes 32:28-32; Kumb 3:18-20).]

13“Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’.

14Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ng'ambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu.

15Mtawasaidia mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowapa ndugu zenu pia mahali pa kupumzikia, kama alivyowapa nyinyi, nao pia wamiliki nchi ambayo wanapewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kisha mtarudi katika nchi ambayo ni mali yenu na kuimiliki, nchi ambayo mlipewa na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, mashariki ya mto Yordani.”

16Wakamjibu Yoshua, “Mambo yote uliyotuamuru tutayafanya, na popote utakapotutuma tutakwenda.

17Kama vile tulivyomtii Mose katika mambo yote, ndivyo tutakavyokutii wewe; Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na Mose.

18Mtu yeyote atakayeasi amri yako au kukataa kutii maneno yako au jambo lolote unalomwamuru, atauawa. Wewe, lakini, uwe na nguvu na kuwa hodari.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania