Mathayo 10

Mathayo 10

Mitume kumi na wawili

(Marko 3:13-19; Luka 6:12-16)

1Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote.[#10:1 Taz maelezo ya Marko 1:23.; #10:1—11:1 Hii ni hotuba ya pili ya Yesu. Baada ya Yesu kuwachagua mitume wake kumi na wawili, anawafundisha na kuwatuma na ujumbe wa kutangaza utawala wa Mungu na hivyo kuwafanya washiriki wake katika kuokoa watu.]

2Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake;[#10:1-2 Ni hapa tu katika Mathayo ambapo wanafunzi au wafuasi 12 wametajwa kama mitume. Yachukuliwa kwamba mitume wanayo mamlaka kutenda na kufanya vitu kwa niaba ya huyo aliyewatuma. Idadi kumi na mbili hapa inawakilisha jumuiya mpya ya watu wa Mungu.]

3Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;[#10:3 Rejea Mat 9:9; taz pia maelezo ya Marko 2:14.; #10:3 Yamkini “Thadayo” ni mtu yuleyule anayetajwa kwa jina “Yuda wa Yakobo” katika Luka 6:16, na Mate 1:13.]

4Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.[#10:4 Au, “Mzelote” hili la pili likiwa ni namna ya Kigiriki ya kutaja Mkanaani, neno ambalo lina maana ya mwenye bidii mno katika mazingira fulani; jina hili si sawa na jina walilopewa wakazi wa Kanaani; taz pia Luka 6:15 maelezo.]

Yesu anawatuma mitume kumi na wawili

(Marko 6:7-13; Luka 9:1-6)

5Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria.[#10:5 Hao walikuwa watu wenye asili ya mchanganyiko ambao walipata kuwako tangu mnamo 721 K.K. baadhi wakiwa watu waliohamishiwa Samaria kutoka Ashuru na wengine kutoka nchi nyingine (taz 2Fal 17:26). Wenyeji wa Samaria, sehemu iliyokuwa kati ya Yudea na Galilaya, hawakupatana na Wayahudi katika mambo ya siasa na mengine ya kidini. Walikuwa na hekalu lao wenyewe ambalo lilikuwa juu ya Mlima Gerizimu. Taz maelezo ya Yoh 4:9.]

6Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.

7Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’

8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure.

9Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba.

10Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake.[#10:10 Au “chakula”. Luka 10:7 ina “mfanyakazi astahili mshahara wake”. Taz pia 1Kor 9:14; 1Tim 5:18.]

11“Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo.

12Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake.

13Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi.[#10:12-13 Ni tafsiri ya neno la Kigiriki “eirene” ambalo latafsiri neno la Kiebrania “shalom” maana yake “amani”. Neno letu la Kiswahili “salamu” (salama) latokana na Kiarabu na kwa kweli maana yake ya msingi ni kumtakia mtu amani, sawa na maana hiyohiyo katika Kiebrania (taz pia Luka 1:28).; #10:13 Ingawa wengine wanafikiri kwa msemo huo Yesu alimaanisha kwamba wao wataendelea kupata baraka, ni dhahiri lakini kwamba maana ya karibu zaidi na mazingira ya maandishi ni kwamba “wao hawatakuwa wamepoteza chochote” au, “haidhuru”.]

14Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung'uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.[#10:14 Kitenda cha ishara cha kuwakataa.]

15Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.[#10:15 Miji ambayo kadiri ya Mwa 19 Mungu aliiteketeza kwa sababu ya uovu mkubwa wa wakazi wake. Katika A.J. (Mat 11:23-24; Luka 17:29; Rom 9:29; 2Pet 2:6; Yuda 7), miji hiyo inatumika kama kitendawili au mfano wa maovu makuu.]

Udhalimu

(Marko 13:9-13; Luka 21:12-17)

16“Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa.

17Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao.

18Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa.

19Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema.

20Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

21“Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.

22Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa.

23“Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.

24“Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumishi hampiti bwana wake.

25Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je, hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?[#10:25 Jina lingine la Shetani, mkuu wa pepo wabaya. Tazama maelezo ya Mat 12:24 na pia Orodha ya Maneno.]

Anayestahili Kuogopwa

(Luka 12:2-7)

26“Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa.[#10:26 Taz maelezo ya Marko 4:22.]

27Ninalowaambieni nyinyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong'onezwa, litangazeni hadharani.

28Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu.[#10:28 Kwa wingi “yule awezaye kuangamiza …” ni Mungu. Rejea Ebr 10:31; Yak 4:12.]

29Shomoro wawili huuzwa kwa sarafu moja ndogo. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu.[#10:29 Ling 6:26; Zab 84:3. Sarafu hiyo ilikuwa ndogo zaidi miongoni mwa sarafu za Kiroma.]

30Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

31Kwa hiyo msiogope; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi.

Kumkiri na kumkana Kristo

(Luka 12:51-53; 14:26-27)

32“Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

33Lakini yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

Mafarakano

(Luka 12:8-9)

34“Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.[#10:34 Picha ya mfano wa kiuandishi yenye maana ya utengano na vurugu.]

35Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake.

36Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.

37“Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.[#10:37 Ingawa Yesu anawataka wafuasi wake kuwaheshimu wazazi wao anaonesha dhahiri kabisa kwamba uhusiano na majukumu ya familia kamwe yasipinge uaminifu kwa Mungu.]

38Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.[#10:38 Msalaba ulikuwa hapo awali chombo cha mateso na ulitumika kutekeleza adhabu ya kifo nyakati za himaya ya Waroma. Aliyehukumiwa kuuawa alibeba msalaba wake mwenyewe hadi mahali ambapo atauawa. Kwa picha hiyo Yesu anawatayarisha wafuasi wake kukikabili kifo hata kujiona kwamba wamekufa kuhusu ulimwengu na wao wenyewe. Rejea pia misemo ya Paulo katika Rom 6:2-11; Gal 2:19; 6:14; Kol 3:3-5.]

39Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.[#10:39 Au, “uhai”. Taz Mat 16:25-26 maelezo.]

Tuzo

(Marko 9:41)

40“Anayewapokea nyinyi, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma.

41Anayempokea nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayempokea mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema.

42Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hakika hatakosa kamwe kupata tuzo lake.”[#10:42 Kutokana na maneno yafuatayo yaani: “kwa sababu ni mfuasi wangu”, wadogo hao si watoto wadogo bali ni msemo wa kuwataja mitume au hata waumini kwa jumla.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania