The chat will start when you send the first message.
1Kisha Mafarisayo na waalimu wa sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza,
2“Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu? Hawanawi mikono ipasavyo kabla ya kula!”[#15:2 Luka 11:38. Yahusu ufafanuzi wa jadi wa sheria ya Mose uliofanywa na waalimu wa Kiyahudi na kusimuliwa kizazi hata kizazi kuhusu kutawadha; taz Marko 7:3 maelezo. Hawanawi mikono ipasavyo: Kama ilivyotakiwa ili kumfanya mtu awe safi kidini, kwa maneno mengine “kutawadha” (15:20).]
3Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe?
4Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’[#15:4 Kuhusu sheria hizo mbili zinazotajwa hapa, taz Kut 20:12; Kumb 5:16.]
5Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’[#15:5 Kiebrania “korbani”. Yaani ni kitu kilichowekwa wakfu kwa Mungu na hivyo hakiwezi kutumiwa namna nyingine (taz maelezo katika Marko 7:11).]
6basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.[#15:6 Hati nyingine za kale kadhaa zina: “baba yake au mama yake”.]
7Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
8‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
9Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”
10Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe![#15:10 Mara kwa mara Mathayo anarudiarudia umuhimu wa kuelewa mafundisho ya Yesu. Jambo hilo linahitaji usikivu, unyenyekevu na utii. Taz 13:13,51; 16:9-12.]
11Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”[#15:11 Ni kitu kimfanyacho mtu kuwa mwiko kidini (Lawi 11). Jambo la kuwa safi na najisi kidini lilitiliwa maanani sana na Wayahudi nyakati za Yesu. Yesu aliweka muundo na msimamo mpya ambao ni kinyume kabisa cha desturi hiyo: uovu uko ndani ya mtu na huo ndio wenye kumfanya mtu kuwa najisi kwelikweli. Huo ni mbaya zaidi; taz Marko 7:2.]
12Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?”
13Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utang'olewa.
14Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.”
15Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.”
16Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi?
17Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni?
18Lakini mambo yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi.
19Maana moyoni hutoka mawazo ya uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa.
20Hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
21Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.[#15:21 Sehemu ambazo zilikaliwa na watu wasio Wayahudi, watu wa mataifa mengine, na ambao Wayahudi waliwaona kuwa watu wasiomjua Mungu.]
22Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.”[#15:22 Jina la sifa la kumtaja Masiha; taz Mat 1:1 maelezo.]
23Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.”[#15:23 Tafsiri nyingine yamkini ni: “Msikilize huyu mama”. Lakini kutokana na maneno ya Yesu: “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”, maneno ambayo yanarudia maoni ya hao wanafunzi kwamba huyu ni mama asiye Myahudi (mbwa), yeye anamwezesha huyo mama kusema ukweli wa hali ilivyo: “hata mbwa huokota …” na kumfanyia huyo mama ombi lake. Yaani, hata wasio Wayahudi watapewa baraka za Kimasiha.]
24Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.”
25Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.”
26Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”[#15:26 Wayahudi waliwaita watu wasio Wayahudi “mbwa”; inaonekana kwamba Yesu, kutokana na maneno ya wanafunzi ya kumtaka amwambie huyo mama aende zake (aya ya 23), anatumia neno hilo anapoongea na huyo mama Mkanaani (asiye Myahudi) kama kwa kejeli, lakini si kwa kupinga kabisa ombi la huyo mama ambaye katika aya ya 27 anasisitiza naye Yesu mwishowe anamjalia ombi lake (aya ya 28). Wasio Wayahudi watashiriki neema za watu wa Mungu kama Wayahudi.]
27Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.”
28Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo.
29Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi.
30Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.
31Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli.
32Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.”
33Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?”
34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.”
35Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini.
36Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu.
37Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba.
38Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.
39Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.[#15:39 Haijulikani ni wapi hasa. Hati nyingine za kale zina: “Magdala”.]