The chat will start when you send the first message.
1Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu,[#2:1 Huu ni mji ulio yapata kilomita 8 kusini mwa Yerusalemu; ulikuwa mji wa kuzaliwa wa mfalme Daudi (1Sam 16:1). Rejea Luka 2:4-7. Wayahudi walitazamia kwamba Mwokozi angezaliwa huko.; #2:1 Anaitwa pia Herode Mkuu. Utawala wa Roma ulimteua kuwa mfalme mwaka wa 40 K.K. lakini alitawala tangu mwaka 37 K.K. mpaka mwaka wa 4 B.K. Alikuwa baba yake Arkelao (taz Mat 2:22), Herode Antipa (taz Mat 14:1) na Filipo (rejea Luka 3:1).; #2:1 Kigiriki ni “magoi”. Tafsiri nyingine yamkini “wanajimu”. Ni vigumu kusema hao walitoka wapi hasa, ila Inaonekana hawakuwa Wayahudi. Hao wanawawakilisha kwa kutangulia watu wasio Wayahudi ambao watamtambua Yesu kuwa Kristo Mwokozi.]
2wakauliza, “Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu.”[#2:2 Katika Hes 24:17 tuna “Nyota itatokea kwa wazawa wa Yakobo”. Kuonekana kwa nyota hiyo kulikuwa kama tangazo kwa hao wataalamu wa nyota kwamba amezaliwa Mwokozi, mfalme wa Wayahudi.]
3Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu.
4Basi, akawaita pamoja makuhani wakuu wote na waalimu wa sheria, akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?”[#2:4 Hawa walikuwa makasisi waliokuwa na jukumu la kusimamia mambo yote ya ibada hekaluni Yerusalemu. Waalimu wa Sheria walikuwa nao wataalamu wa mafundisho na maagizo ya sheria za Agano la Kale.]
5Nao wakamjibu, “Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika:
6‘Ee Bethlehemu nchini Yudea,
wewe si mdogo kamwe kati ya miji maarufu ya Yudea;
maana kwako atatokea kiongozi
atakayewaongoza watu wangu, Israeli.’”
7Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea.
8Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, “Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende kumwabudu.”
9Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto.
10Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno.
11Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani na manemane.[#2:11 Au “uvumba”. Huo ulitumika katika kutambikia. Yafaa kukumbuka hapa kwamba zawadi hizo zilifaa kwa mfalme na siyo kwa mtu wa kawaida.; #2:11 Haya yalitengenezwa kutoka utomvu wa mti fulani, nayo yalitumika kama marashi na mara nyingine tunaambiwa kwamba yalichanganywa katika divai na kupewa mtu ili kumpunguzia maumivu. Aghalabu yalitumika kupaka maiti.]
12Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.
13Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokuambia, maana Herode anakusudia kumuua huyu mtoto.”
14Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri.
15Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie:
“Nilimwita Mwanangu kutoka Misri.”
16Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota.
17Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:
18“Sauti imesikika huko Rama,
kilio na maombolezo mengi.
Raheli anawalilia watoto wake,
wala hataki kutulizwa,
maana wote wamefariki.”
19Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri,
20akamwambia, “Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumuua mtoto huyo wamekwisha kufa.”
21Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea nchini Israeli.
22Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya,[#2:22 Huyu alikuwa mwanawe Herode Mkubwa. Alitawala tangu mwaka wa 4 K.K. hadi mwaka 6 B.K. kule Yudea, Samaria na Idumea. Alitawala mahali pa baba yake yaani Herode ambaye alikufa mnamo mwaka wa 4 K.K. Kwa vile Arkelao hakuwa na madaraka juu ya eneo la Galilaya Yosefu, Maria na mwanawe wangeweza kukaa huko kwa usalama.]
23akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii:
“Ataitwa Mnazare.”