The chat will start when you send the first message.
1Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumuua.[#27:1 Taz Mat 26:57 maelezo.]
2Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.[#27:2 Huyu alikuwa mtawala wa Kiroma au gavana. Alitawala huko Yudea mnamo mwaka 26-36 B.K. Taz Mat 27:11 maelezo.]
3Hapo, Yuda, ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu vile vipande thelathini vya fedha.
4Akawaambia, “Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe.” Lakini wao wakasema, “Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako.”
5Naye akazitupa zile fedha hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.
6Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya hekalu kwa maana ni fedha za damu.”
7Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
8Ndio maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.
9Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walichukua vipande thelathini vya fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walimtia bei,[#27:9b-10 Maneno yamekaririwa kutoka Zek 11:12-13 pamoja na mengine kutoka Yer 18:2-3; 19:1-2; 32:6-15.]
10wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.”
11Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.”[#27:11 Swali la Pilato na jibu la Yesu ni kama lile swali na jibu wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu katika Mat 26:63-64. Jibu “Wewe umesema” laweza kueleweka kama “Ndiyo” au kwamba Yesu anakubali kuwa yeye ni mfalme lakini si kwa maana anayofikiria Pilato. Taz Mat 26:64 maelezo.]
12Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.
13Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?”
14Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.[#27:12-14 Isa 53:7; Mat 26:63; Luka 23:9; Yoh 19:19.]
15Ilikuwa kawaida wakati wa sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.
16Wakati huo kulikuwa na mfungwa aliyejulikana sana, jina lake Baraba.[#27:16 Hati nyingine za kale zina jina “Yesu” kabla ya jina Baraba kama ilivyo katika aya ifuatayo.]
17Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwaye Kristo?”
18Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.
19Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
20Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.
21Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!”
22Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!”
23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!”
24Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.”[#27:24 Kama ishara ya kutokuwa na hatia (Kumb 21:6-9; Zab 26:6).]
25Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”[#27:25 Yaani wako tayari kulaumiwa kutokana na kifo hicho (taz 2Sam 1:13-16; 3:29; Yer 51:35 n.k. kuhusu namna hii ya kusema).]
26Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe.
27Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.
28Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.
29Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!”
30Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.
31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
32Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.[#27:32 Mji uliopo pwani ya Afrika Kaskazini.; #27:32-56 Mwandishi anarudiarudia yaliyomo katika Zab 22 na Zaburi nyingine ambazo aliziona kuwa zenye ujumbe wa kinabii kuhusu kifo cha Yesu.]
33Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa,[#27:33 Labda paliitwa hivyo kwa sababu palikuwa kilima ambacho kilionekana hivyo.]
34wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.[#27:34 Zab 69:21.]
35Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.[#27:35 Maneno yanayokumbusha Zab 22:18.]
36Wakaketi, wakawa wanamchunga.
37Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.”[#27:37 Ilikuwa kawaida kutangaza hadharani kosa la mtu aliyehukumiwa kuuawa. Katika kisa hiki cha Yesu, ilani hiyo aliyowekewa inaonekana kuwa ya uhaini kwani inaonesha au kuwafanya watu wafikiri alijitakia kuwa mfalme.]
38Wanyang'anyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
39Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,[#27:39 Mwandishi anatumia picha ya Zab 22:7; rejea Zab 109:25.]
40“Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!”
41Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema,
42“Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.
43Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.”[#27:43 Maneno haya yamekaririwa kutoka Zab 22:8.]
44Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
45Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote.
46Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”[#27:46 Maneno ya kwanza ya Zab 22:1. “Eli” ni Kiebrania maana yake “Mungu wangu”; na “lema sabakthani” ni Kiaramu, maana yake “Mbona umeniacha”.]
47Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.”[#27:47 Wayahudi walitumaini kurudi kwa nabii Elia na waliamini kwamba Elia angekuja kuwasaidia wanaoteseka (rejea aya 49). Taz Mat 16:14 maelezo.]
48Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.[#27:48 Kitendo ambacho kinakumbusha Zab 69:21.]
49Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.”
50Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
51Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;[#27:51 Tukio hili la kupasuka pazia la hekalu, kulingana na Ebr 9:19; 9:3-12; 10:19-20, limefafanuliwa kama ishara ya uhuru wa kumwendea Mungu sasa bila kizuizi kwa njia ya kifo chake Yesu Kristo.]
52makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;
53nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
54Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
55Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.[#27:55 Yaani tangu wakati ule Yesu alipoanza mahubiri yake kule Galilaya (rejea Luka 8:1-3).; #27:55-56 Luka 8:2 maelezo.]
56Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.[#27:56 Rejea Mat 4:21 na taz 20:20 maelezo. Kuhusu watu wengine wanaotajwa hapa taz maelezo katika Marko 15:40.]
57Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Arimathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
58Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.
59Yosefu akauchukua ule mwili, akauzungushia sanda safi ya kitani,
60akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.[#27:60 Wayahudi wengine walikuwa na desturi ya kuzika maiti wao kwenye nafasi zilizochongwa miambani kisha wakafunika kwa jiwe kubwa la mviringo ambalo waliliviringishia kwenye mahali pa kuingia.]
61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.[#27:61 Yahusu wale Maria wawili wa aya ya 56.]
62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,[#27:62 Yaani siku ya Ijumaa ambayo iliitwa hivyo kwa kuwa Wayahudi walijitayarisha kuadhimisha siku iliyofuata ya Sabato.]
63Wakasema, “Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’[#27:63 16:21; 17:23; 20:19; Marko 8:31; 9:31; 10:33-34; Luka 9:22; 18:31-33.]
64Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali.”
65Pilato akawaambia, “Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo.”
66Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.