Hesabu 25

Hesabu 25

Waisraeli na Baali wa Peori

1Waisraeli walipokuwa huko Shitimu, wanaume walianza kuzini na wanawake wa Moabu.[#25:1 Yamkini ni jina la mahali au eneo ambapo Waisraeli walianza kuivamia nchi ya Kanaani. Eneo hilo lilikuwa upande wa mashariki ya Mto Yordani mkabala na mji wa kale wa Yeriko (taz 22:1; 33:49; Yos 2:1).]

2Wanawake hao waliwaalika Waisraeli washiriki matambiko waliyotambikia miungu yao, nao Waisraeli wakala chakula na kuiabudu miungu yao.

3Ndivyo Waisraeli walivyojiunga na mungu Baali wa Peori, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yao.[#25:2-3 Zab 106:28-29; Hos 9:10. “Baali” lilikuwa jina la miungu kadhaa ya rutuba ambayo iliabudiwa mahali pengi katika maeneo hayo ya Mashariki ya Kati ya Kale. Mmoja wa hiyo miungu ni huyu Baali wa Peori. “Peori” lilikuwa jina la mahali hapo ambapo huyo Baali aliabudiwa.]

4Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wachukue viongozi wote wa Israeli, uwanyonge mbele yangu juani, ili ghadhabu yangu dhidi yenu ipite.”[#25:4 Yamkini ni viongozi wale waliowaongoza hao watu kutenda uovu. Baadhi wanafikiri “viongozi” (Kiebrania ni neno “rosh” - kichwa) huenda lilikuwa limeandikwa kwa konsonanti ambazo lingekuwa na maana ya “waovu”.]

5Mose akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu amuue mtu yeyote miongoni mwenu ambaye amejiunga na mungu Baali wa Peori.”

6Wakati huohuo mtu mmoja akamleta mwanamke mmoja Mmidiani nyumbani kwake, Mose na jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wanaomboleza penye lango la hema la mkutano.[#25:6 Yaelekea wakati huo Waisraeli hawakuruhusiwa kuoana na watu wa makabila mengine (ling Ezra 10:1—11:44); ingawa hapo awali Abrahamu alimwoa Hagari Mmisri (Mwa 16:1-4) naye Mose alimwoa Zipora Mkushi (Kut 2:21) na Boazi alimwoa Ruthu Mmoabu (Rut 4:1-21).]

7Basi, Finehasi mwana wa Eleazari mwana wa kuhani Aroni alipoona hayo, aliinuka akatoka katika hiyo jumuiya, akachukua mkuki

8na kumfuatia yule Mwisraeli mpaka hemani, akawachoma mkuki wote wawili tumboni. Maradhi mabaya yaliyokuwa yamewaangamiza Waisraeli yakakomeshwa.

9Waliokufa kutokana na maradhi yale mabaya walikuwa watu 24,000.

10Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

11“Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, ameizuia hasira yangu dhidi ya Waisraeli; miongoni mwenu ni yeye tu aliyeona wivu kama nilio nao mimi. Ndio maana sikuwaangamiza Waisraeli wote kwa hasira yangu.

12Kwa hiyo mwambie kwamba ninafanya naye agano la amani.

13Naagana naye kwamba yeye na wazawa wake watakuwa makuhani milele kwa sababu aliona wivu kwa ajili yangu, Mungu wake, akawafanyia upatanisho Waisraeli.”

14Huyo Mwisraeli aliyeuawa pamoja na mwanamke wa Kimidiani aliitwa Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa mojawapo katika kabila la Simeoni.

15Na huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa aliitwa Kozbi binti Suri, aliyekuwa kiongozi wa ukoo fulani huko Midiani.

16Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

17“Wachokoze Wamidiani na kuwaangamiza,

18kwa sababu waliwachokoza nyinyi kwa hila zao, wakawadanganya kuhusu jambo la Peori, na kwa sababu ya Kozbi, binti yao, aliyeuawa wakati maradhi mabaya yalipozuka kule Peori.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania