Zaburi 137

Zaburi 137

Ombolezo ugenini

1Kando ya mito ya Babuloni, tulikaa,[#137:1 Yaani mifereji na vijito vya mito ya Tigri na Eufrate.]

tukawa tunalia tulipokumbuka Siyoni.

2Katika miti ya nchi ile,

tulitundika zeze zetu.

3Waliotuteka walitutaka tuwaimbie;

watesi wetu walitutaka tuwafurahishe:

“Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Siyoni!”

4Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu

katika nchi ya kigeni?

5Ee Yerusalemu, kama nikikusahau,

mkono wangu wa kulia na ukauke!

6Ulimi wangu na uwe mzito,

kama nisipokukumbuka wewe, ee Yerusalemu;

naam, nisipokuthamini kuliko furaha yangu kubwa!

7Ee Mwenyezi-Mungu, usisahau waliyotenda Waedomu,[#137:7 Huenda Waedomu walifurahi wakati mji wa Yerusalemu ulipoteketezwa na Wababuloni na wengi wa wakazi wake wakachukuliwa mateka. Taz Eze 35:5-15; Oba 10-14.]

siku ile Yerusalemu ilipotekwa;

kumbuka waliyosema:

“Bomoeni mji wa Yerusalemu!

Ng'oeni hata na misingi yake!”

8Ee Babuloni, utaangamizwa!

Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotutenda!

9Heri yule atakayewatwaa watoto wako

na kuwapondaponda mwambani!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania