The chat will start when you send the first message.
1Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi.[#14:1 Hapo awali alikwisha sema kuwa wakaribisheni (taz Rom 12:13) wazo analolijenga juu ya onyo la Yesu kuhusu kukaribisha watu (taz Mat 22:31-46). Paulo anawashauri wasiwe na ubaguzi kwa yeyote hata kwa yule aliye dhaifu kiimani.]
2Watu hutofautiana: mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani.[#14:2-3 Mkazo kuhusu vyakula unatokana na mabishano yaliyokuwepo bila shaka kati ya Wakristo Wayahudi na Wakristo wa mataifa mengine; hali hii ilitokeza kudharauliana. Paulo anasisitiza kuwa mambo ya vyakula yasivuruge uhusiano wao au upendo kati yao hata wakakwazana.]
3Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali.
4Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha.[#14:4 Aya hii inakaza kule kutohukumiana au kuoneana kinyongo (taz pia 7:1).; #14:4 Iliaminiwa kati ya Waisraeli kuwa Mungu ana uwezo wa kushusha wenye nguvu na kuinua wanyonge au wadhaifu. Paulo ananukuu maneno ya mtunga Zaburi 113 (taz Zab 113:7; ling 1Sam 2:8; Zab 9:2,18; 140:12).]
5Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake.[#14:5-10 Maelezo zaidi kuhusu kutodharauliana au kuhukumiana kwa ajili ya chakula.]
6Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu.
7Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe[#14:7-8 Kutegemeana kwa wanadamu kunakazwa naye Paulo. Ni kama maendelezo ya hoja yake ya kwamba Wakristo wasibaguane, wapendane kwa kutumia vipawa vyao na kukubali tofauti za mapokeo waliyo nayo.]
8maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana.[#14:8 Kuishi au kufa kunakotajwa kunagusa maisha ya Mkristo hapa ulimwenguni, ni kama alivyokwisha sema kuwa wamvae Kristo (13:14) na ni huyo anayetajwa kuwa alikufa akafufuka kwa ajili ya watu wote. Mtu akimvaa Kristo akatenda matakwa ya Mungu, yaani akawa na upendo kwa wengine huyo hajiishii, bali anatimiza agizo la Mungu naye Yesu Kristo - wazo ambalo Paulo amekwisha dokeza katika 13:9 (taz maelezo ya 13:9).]
9Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa walio hai na wafu.
10Kwa nini basi, wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.[#14:10-12 Swali ambalo halihitaji majibu, naye amekwisha lirudia mara nyingi katika sura hii (taz 2:1,3; 12:19-20; 14:4 ling 8:33). Hukumu ni ya Mungu, ndivyo Paulo anavyoshauri (taz pia 12:19-20).]
11Maana Maandiko yanasema:
“Kama niishivyo, asema Bwana,
kila mtu atanipigia magoti,
na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu.”
12Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja juu yake mwenyewe mbele ya Mungu.[#14:12 Ni ufupisho wa mafundisho au maelekezo yake.]
13Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu au kumsababisha aanguke katika dhambi.[#14:13-18 Maelekezo zaidi kuhusu upendo - namna nzuri ya Wakristo kuishi pamoja. Kufuata mafundisho ya Paulo kuhukumu na kudharau ni matendo yanayokwaza watu na kuwahuzunisha.]
14Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi.
15Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na upendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake!
16Basi, msikubali kitu mnachokiona kwenu kuwa chema kidharauliwe.
17Maana ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.[#14:17 Paulo anatumia maneno yaliyo na uhusiano na yale Yesu aliyomwambia Shetani: “Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu.” (Taz Mat 4:4; Luka 4:4).; #14:17 Mambo matatu ambayo Paulo anashauri Wakristo wayazingatie, wawe nayo kati yao wenyewe na pia kati yao na watu wengine na hasa kati ya Wakristo Wayahudi na Wakristo wa mataifa mengine. Mkazo huohuo anaurudia katika 15:13. Na katika mtiririko huohuo wa mawazo anakaza katika barua yake kwa Wagalatia (taz Gal 5:22) ingawa hapo Paulo hataji kwa wazi neno uadilifu. Nao Wakristo anawashauri wazingatie mambo hayo (taz 2Kor 13:11). Paulo anasisitiza kuwa hivi vyote vinaletwa na Roho Mtakatifu ni kusema kuwa Roho ana kazi ndani ya muumini. Kwa hiyo mtu akiwa nayo ametimiza matakwa ya Roho; naye Roho anaishi ndani yake (taz 8:9-11).]
18Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu.[#14:18 Maelezo ya Paulo kuhusu anyemtumikia Kristo yaelekea yana msingi katika maneno ya mwandishi wa Injili ya Mathayo aliyoandika akisema kuwa Kristo alikuwa akimpendeza Mungu na watu mfano unaopaswa kuigwa na mtumishi wa Kristo.]
19Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana.[#14:19 Yaani kusaidiana. Dhaifu kiimani kusaidiwa na asiye dhaifu na kwa kutumia vipawa kusaidiana si kimwili tu hata kiroho (taz 1:11-12). Wazo hili la kujengana Paulo analieleza hata katika barua yake kwa Wakorintho (taz 1Kor 12) anakokaza kuwa Wakristo ni viungo vya mwili mmoja wa Kristo (ling Rom 12:4; 1Kor 10:17; 12:13,20; Efe 4:4; Kol 3:15).]
20Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi.[#14:20 Kutoridhika na hali ile ya kumvumilia mwingine afanye analotaka - ale chochote anachopenda. Yaelekea kati ya Waroma kulikuwepo mgongano mkubwa kati ya Waamini kwa ajili ya chakula. Mgongano huohuo ulikuwa kati ya Wakorintho. Kwa Wakorintho alitoa maelezo marefu kuhusu chakula (taz 1Kor 8:1-13).; #14:20 Swali laweza kuulizwa ‘Mtu awezaje kuanguka dhambini ikiwa mwingine anakula chakula cha namna fulani?’ Hapa Paulo anataka kukazia hoja yake kuwa kama kuna chakula ambacho, k.m. kilitolewa kwa miungu na mkristo fulani akala kwa kuwa yeye anaona hakuna shida, kwani haabudi miungu hiyo, basi, mwingine atakwazika atakuwa na chuki au huenda anaweza naye akala na huku akaamua pia kuabudu miungu hiyo badala ya Mungu wa kweli na Mwokozi wake Yesu Kristo.]
21Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke.[#14:21 Upendo kwa mwingine Paulo anashauri kuwa, umsukume aache chakula hata kama ni kitamu namna gani ili asimkwaze. Mawazo hayohayo Paulo anayatoa katika barua yake kwa Wakorintho akijieleza kuwa yeye yu tayari kuacha chakula fulani asimkwaze mwingine asiyekula chakula hicho (taz 1Kor 8:13).]
22Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake.
23Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.