The chat will start when you send the first message.
1Sanduku la Bwana lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,
2Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Bwana ? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”
3Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”
4Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?”
Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni hiyo hiyo imewadhuru ninyi na watawala wenu.
5Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mtukuzeni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.
6Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?
7“Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.
8Chukueni hilo Sanduku la Bwana na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea Bwana kama sadaka ya hatia. Lipelekeni,
9lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litaenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba Bwana ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa Bwana uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”
10Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.
11Wakaliweka Sanduku la Bwana juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.
12Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
13Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.
14Lile gari la kukokotwa lilikuja kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana .
15Walawi walilishusha Sanduku la Bwana , pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Bwana .
16Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi Ekroni siku ile ile.
17Haya ndio yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwa Bwana : moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.
18Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao yenye ngome, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku la Bwana , ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.
19Lakini Mungu aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-Shemeshi, akiwaua watu sabini miongoni mwao kwa sababu walichungulia ndani ya Sanduku la Bwana . Watu wakaomboleza kwa sababu ya pigo zito kutoka kwa Bwana ,
20nao watu wa Beth-Shemeshi wakauliza, “Ni nani awezaye kusimama mbele za Bwana , huyu Mungu aliye mtakatifu? Sanduku litapanda kwenda kwa nani kutoka hapa?”
21Kisha wakatuma wajumbe kwa watu wa Kiriath-Yearimu, wakisema, “Wafilisti wamerudisha Sanduku la Bwana . Shukeni na mlipandishe huko kwenu.”