The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia kusema:
2“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Mlima Seiri, utabiri dhidi yake
3na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Mimi ni kinyume nawe, ee Mlima Seiri, nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya ukiwa.
4Nitaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa ukiwa. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana .
5“ ‘Kwa sababu ulificha moyoni uadui wa siku nyingi nawe ukawatoa Waisraeli wauawe kwa upanga wakati wa maafa yao, wakati adhabu yake ilipofikia kilele chake,
6kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, nitakutia katika umwagaji damu nao utakufuatia. Kwa kuwa hukuchukia kumwaga damu, kumwaga damu kutakufuatia.
7Nitaufanya Mlima Seiri ukiwa na kuukatilia mbali na wote wanaokuja na wanaoenda.
8Nitaijaza milima yenu kwa watu wake waliouawa, wale waliouawa kwa upanga wataanguka juu ya vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo yako yote.
9Nitakufanya ukiwa milele, watu hawataishi katika miji yako. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana .
10“ ‘Kwa sababu umesema, “Mataifa haya mawili na nchi hizi zitakuwa zetu nasi tutazimiliki,” ingawa hata Mimi Bwana nilikuwa huko,
11kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, nitakutenda kwa kadiri ya hasira na wivu uliouonesha katika chuki yako juu yao nami nitafanya nijulikane miongoni mwao wakati nitakapokuhukumu.
12Ndipo utakapojua kuwa Mimi Bwana nimesikia mambo yote ya dharau uliyosema dhidi ya milima ya Israeli. Ulisema, “Wamefanyika ukiwa na kutiwa mikononi mwetu tuwararue.”
13Ulijigamba dhidi yangu na kusema maneno dhidi yangu bila kujizuia, nami nikayasikia.
14Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Dunia yote inaposhangilia, nitakufanya ukiwa.
15Kwa sababu ulishangilia wakati urithi wa nyumba ya Israeli ulipofanyika ukiwa, hivyo ndivyo nitakavyokutendea. Utakuwa ukiwa, ee Mlima Seiri, wewe na Edomu yote. Kisha ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana .’ ”