Waamuzi 3

Waamuzi 3

Mataifa yaliyobaki katika nchi

1Haya ndio mataifa ambayo Bwana aliyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakushiriki vita yoyote huko Kanaani

2(alifanya hivi ili tu kuwafundisha vita wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa na uzoefu wa vita hapo awali):

3watawala watano wa Wafilisti, pamoja na Wakanaani wote, Wasidoni, na Wahivi walioishi katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi.

4Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli, kuona kama wangetii amri za Bwana , alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Musa.

5Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

6Wakaoa binti za hao mataifa, na wakawatoa binti zao wenyewe waolewe na wana wa hao mataifa, na wakaitumikia miungu yao.

Othnieli

7Waisraeli wakafanya maovu machoni pa Bwana , wakamsahau Bwana Mungu wao na kutumikia Mabaali na Maashera.

8Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli. Hivyo akawauza mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao Waisraeli wakamtumikia kwa muda wa miaka nane.

9Waisraeli walipomlilia Bwana , yeye akawainulia mkombozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa.

10Roho wa Bwana akaja juu yake; hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, na akaenda vitani. Bwana akamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda.

11Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, hadi Othnieli mwana wa Kenazi alipofariki.

Ehudi

12Waisraeli wakafanya maovu mbele za Bwana tena; na kwa kuwa walifanya maovu hayo, Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli.

13Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki kwake, wakashambulia Israeli, na wakatwaa Mji wa Mitende.[#3:13 yaani Yeriko]

14Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na nane.

15Waisraeli wakamlilia tena Bwana , naye akawapa mkombozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi.

16Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga ukatao kuwili, ukiwa na urefu wa kama dhiraa moja, naye akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake, kwenye paja lake la mkono wa kuume.[#3:16 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.]

17Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, aliyekuwa mtu mnene sana.

18Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, akawatuma wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru waende zao.

19Ehudi akafuatana nao hadi kwenye sanamu za mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwako.”

Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.

20Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kiti chake,

21Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake.

22Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga.

23Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu, na kuifunga kwa funguo.

24Baada yake kuondoka, watumishi wakaja na kupata milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka anajisaidia chumba cha ndani.”

25Wakangoja hadi wakawa na fadhaa, na wakati hakuifungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama, wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.

26Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira.

27Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.

28Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Bwana amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakumwacha mtu yeyote kuvuka.

29Wakati huo wakawaua Wamoabu wapatao elfu kumi wenye nguvu na mashujaa; hakuna yeyote aliyetoroka.

30Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.

Shamgari

31Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti mia sita kwa fimbo ya ngʼombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.