Yoshua 11

Yoshua 11

Wafalme wa kaskazini washindwa

1Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari hizo, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu,

2na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, katika Shefela, na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi;[#11:2 au upande wa magharibi chini ya vilima]

3kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika eneo ya Mispa.

4Wakaja na vikosi vyao vyote na idadi kubwa ya farasi na magari ya vita: jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari.

5Wafalme hawa wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja kwenye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli.

6Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao ya vita.”

7Hivyo Yoshua na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula kwenye Maji ya Meromu na kuwashambulia,

8naye Bwana akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hata pakawa hakuna yeyote aliyebaki.

9Yoshua akawatendea kama Bwana alivyoamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao ya vita.

10Wakati huo Yoshua akarudi na kuuteka mji wa Hazori na kumuua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.)

11Kila aliyekuwa ndani yake wakamuua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza chochote chenye pumzi, na akauchoma Hazori kwa moto.

12Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake, na akawaua kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, jinsi Musa mtumishi wa Bwana alivyowaagiza.

13Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji iliyojengwa katika vilima vyao vidogo, isipokuwa mji wa Hazori, ambao Yoshua aliuchoma kwa moto.

14Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, pasipo kumbakiza yeyote mwenye pumzi.

15Kama vile Bwana alivyomwagiza Musa mtumishi wake, vivyo hivyo Musa alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya vivyo hivyo; hakukosa kufanya lolote katika yale yote Bwana aliyomwagiza Musa.

16Yoshua akaiteka nchi hii yote: nchi ya vilima, Negebu yote, eneo yote ya Gosheni, na Shefela, Araba na milima ya Israeli pamoja na materemko yake,

17kuanzia Mlima Halaki ambao umeinuka kuelekea Seiri hadi Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni chini ya Mlima Hermoni. Akawateka wafalme wake wote, akawapiga na kuwaua.

18Yoshua akapigana vita dhidi ya wafalme hawa wote kwa muda mrefu.

19Hakuna mji wowote katika eneo hili uliofanya mkataba wa amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa katika vita.

20Kwa maana Bwana mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, awafutilie mbali pasipo huruma, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

21Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka nchi yote ya vilima ya Yuda, na kutoka nchi yote ya vilima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao.

22Hakuna Waanaki waliosalia katika eneo la Waisraeli; ila tu, kuna wachache waliosalia katika maeneo ya Gaza, Gathi na Ashdodi.

23Hivyo Yoshua akaiteka nchi hiyo yote kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Musa, naye Yoshua akawapa Israeli kuwa urithi wao, kulingana na walivyogawanyika katika makabila yao.

Ndipo nchi ikawa na amani bila vita.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.