Yoshua 22

Yoshua 22

Makabila ya mashariki kurudi nyumbani

1Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase,

2naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Musa mtumishi wa Bwana aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru.

3Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi Bwana Mungu wenu aliyowapa.

4Sasa kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwapa ngʼambo ya Yordani.

5Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria ambazo Musa mtumishi wa Bwana aliwapa: yaani kumpenda Bwana Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.”

6Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani kwao.

7(Kwa nusu ya kabila la Manase, Musa alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi mwa Yordani pamoja na ndugu zao.) Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki,

8akisema, “Rudini nyumbani kwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia mavazi mengi; nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.”

9Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la Bwana kupitia Musa.

10Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani.

11Waisraeli hao wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi karibu na Yordani kwenye upande wa Israeli,

12Waisraeli hao wengine walikusanyika huko Shilo ili wapigane nao.

13Kwa hiyo Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, aende katika nchi ya Gileadi kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase.

14Wakatuma viongozi kumi pamoja naye, mmoja kutoka kwa kila kabila la Israeli, kila mmoja akiwa kiongozi katika jamaa miongoni mwa koo za Israeli.

15Walipofika Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia:

16“Kusanyiko lote la Bwana wasema hivi: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli jinsi hii? Mmewezaje kumwacha Bwana na kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi?

17Je, dhambi ya Peori haikutosha? Hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la Bwana , hadi leo hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo!

18Je, sasa ndiyo mnamwacha Bwana ?

“ ‘Mkimwasi Bwana leo, kesho atawakasirikia kusanyiko lote la Israeli.

19Ikiwa nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya Bwana , mahali Maskani ya Bwana ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya Bwana wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu, isipokuwa madhabahu ya Bwana Mungu wetu.

20Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, je, ghadhabu haikuwapata kusanyiko lote la Israeli? Si yeye pekee aliyekufa kwa ajili ya dhambi yake.’ ”

21Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema:

22“Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana ! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana ! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa Bwana , msituache hai siku hii ya leo.

23Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha Bwana , na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, Bwana mwenyewe na atupatilize leo.

24“Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na Bwana , Mungu wa Israeli?

25Bwana ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa Bwana .’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha Bwana .

26“Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’

27Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu Bwana katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika Bwana .’

28“Nasi tulisema, ‘Wakati wowote wakituambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya Bwana , ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’

29“Hili jambo la kumwasi Bwana na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, isipokuwa madhabahu ya Bwana Mungu wetu iliyo mbele ya Maskani yake na liwe mbali nasi.”

30Kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko, hao wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika.

31Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba Bwana yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa Bwana katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli kutoka kwa mkono wa Bwana .”

32Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, na viongozi wakarudi Kanaani kutoka mkutano wao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi, nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli.

33Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.

34Nao Wareubeni na Wagadi wakaita madhabahu hayo Edi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba Bwana ndiye Mungu.[#22:34 yaani Shahidi]

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.