The chat will start when you send the first message.
1Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli.
2Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki mwa Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.
3Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.”
4Basi wakapanda kama wanaume elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na wanaume wa Ai,
5ambao waliwaua wanaume kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye miteremko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka kwa hofu, ikawa kama maji.[#7:5 au machimbo ya mawe]
6Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana , na akabakia hapo hadi jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo, wakatia mavumbi vichwani mwao.
7Yoshua akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani!
8Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake?
9Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”
10Bwana akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini ukilala kifudifudi?
11Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; wameiba, wamesema uongo, na wameviweka pamoja na mali yao.
12Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena hadi mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.
13“Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa ajili ya kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Bwana , Mungu wa Israeli: Vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa vimo kati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu hadi mtakapoviondoa.
14“ ‘Asubuhi, mtakuja kabila kwa kabila. Kisha kabila atakalolichagua Bwana watakuja mbele kufuatana na koo zao; nao ukoo atakaouchagua Bwana watakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa atakayoichagua Bwana watakuja mbele mtu kwa mtu.
15Yule atakayekutwa na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, atateketezwa kwa moto pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ”
16Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na kabila la Yuda likachaguliwa.
17Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawachagua Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikachaguliwa.
18Yoshua akaamuru jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akachaguliwa.
19Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana , Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”
20Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana , Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya:
21Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”[#7:21 Shekeli 200 ni sawa na kilo 2.3.; #7:21 Shekeli 50 ni sawa na gramu 600.]
22Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakakimbia hadi kwenye hema. Tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa kwenye hema lake, pamoja na ile fedha chini yake.
23Wakavichukua vile vitu toka kwenye hema, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakavitandaza mbele za Bwana .
24Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe wa kiume na wa kike, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema lake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori.
25Yoshua akasema, “Kwa nini umetuletea taabu hii? Bwana atakuletea taabu leo.”
Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto.
26Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo hadi leo. Naye Bwana akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori tangu siku hiyo.[#7:26 maana yake Bonde la Taabu]