Yoshua 9

Yoshua 9

Udanganyifu wa Wagibeoni

1Basi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia haya yote, na wale waliokuwa katika nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika pwani yote ya Bahari Kuu hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi),[#9:1 au upande wa magharibi chini ya vilima; #9:1 yaani Bahari ya Mediterania]

2waliungana ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli.

3Hata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia kuhusu yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai,

4waliamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo ya magunia yaliyochakaa, na viriba vikuukuu vya mvinyo, vyenye nyufa zilizozibwa.

5Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa, kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga.

6Ndipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali, wakamwambia yeye pamoja na Waisraeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali; fanyeni mkataba nasi.”

7Basi Waisraeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi. Twawezaje basi kufanya mkataba nanyi?”

8Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.”

Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, na mnatoka wapi?”

9Nao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa Bwana Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri,

10pia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi.

11Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’

12Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu.

13Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.”

14Basi Waisraeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa Bwana .

15Ndipo Yoshua akafanya nao mkataba wa amani ili kuwaacha waishi, na viongozi wa kusanyiko wakauthibitisha kwa kiapo.

16Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao.

17Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu.

18Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Bwana , Mungu wa Israeli.

Kusanyiko lote wakanungʼunika dhidi ya hao viongozi,

19lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Bwana , Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa.

20Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.”

21Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.

22Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi?

23Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”

24Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Bwana Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili.

25Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.”

26Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua.

27Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana mahali pale Bwana angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.