The chat will start when you send the first message.
1“ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana:
2Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, nayo damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu.
3Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia, na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani,
4figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozifunika karibu na kiuno, na kipande kirefu cha ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo.
5Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia.
6Mwanaume yeyote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu; ni takatifu sana.
7“ ‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawasawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho.
8Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuichukua ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake.
9Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaango itakuwa ya kuhani anayeitoa.
10Nayo kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au iko kavu, itakuwa ya wana wa Haruni, nayo itagawanywa sawa kati yao.
11“ ‘Haya ndio masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa Bwana :
12“ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu na iliyopakwa mafuta, na maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta.
13Pamoja na sadaka yake ya amani ya shukrani, ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu.
14Ataleta moja ya kila aina ya andazi kuwa sadaka, matoleo kwa Bwana ; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani.
15Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku hiyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote hadi asubuhi.
16“ ‘Lakini ikiwa sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini chochote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake.
17Nyama yoyote ya sadaka inayobaki hadi siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto.
18Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, Bwana hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi. Mtu atakayekula sehemu yake yoyote atahesabiwa hatia.
19“ ‘Nyama inayogusa chochote kilicho najisi kamwe haitaliwa; lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu yeyote aliyetakaswa anaweza kuila.
20Lakini kama mtu yeyote najisi akila nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Bwana , huyo mtu lazima akatiliwe mbali na watu wake.
21Kama mtu yeyote akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu chochote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Bwana , mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
22Bwana akamwambia Musa,
23“Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ngʼombe, kondoo wala mbuzi.
24Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na wanyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale.
25Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa Bwana kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
26Popote mtakapoishi, kamwe msile damu ya ndege yeyote wala ya mnyama.
27Mtu yeyote atakayekula damu lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”
28Bwana akamwambia Musa,
29“Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote aletaye sadaka ya amani kwa Bwana ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa Bwana .
30Ataleta sadaka kwa mikono yake mwenyewe iliyotolewa kwa Bwana kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
31Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Haruni na wanawe.
32Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo.
33Mwana wa Haruni atoaye damu na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake.
34Kutoka kwa sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa, pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Haruni na wanawe kuwa fungu lao la milele kutoka kwa Waisraeli.’ ”
35Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, ambazo zilitengwa kwa ajili ya Haruni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu ili kumtumikia Bwana katika kazi ya ukuhani.
36Siku ile walipopakwa mafuta, Bwana aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la milele kwa vizazi vijavyo.
37Basi haya ndio masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu, na sadaka ya amani,
38ambayo Bwana alimpa Musa juu ya Mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa Bwana , katika Jangwa la Sinai.