Zaburi 10

Zaburi 10

Zaburi 10

Sala kwa ajili ya haki

1Kwa nini, Ee Bwana , unasimama mbali?

Kwa nini unajificha wakati wa shida?

2Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini,

waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.

3Hujivunia tamaa za moyo wake;

humbariki mlafi na kumtukana Bwana .

4Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu,

katika mawazo yake yote

hakuna nafasi ya Mungu.

5Njia zake daima hufanikiwa;

hujivuna na amri zako ziko mbali naye,

huwacheka kwa dharau adui zake wote.

6Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa,

daima nitakuwa na furaha,

kamwe sitakuwa na shida.”

7Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho;

shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.

8Huvizia karibu na vijiji;

kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia,

akivizia wapitaji.

9Huvizia kama simba aliye mawindoni;

huvizia kumkamata mnyonge,

huwakamata wanyonge na kuwaburuza

katika wavu wake.

10Mateka wake hupondwa, huzimia;

wanaanguka katika nguvu zake.

11Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau,

huficha uso wake na haoni kabisa.”

12Inuka Bwana ! Inua mkono wako, Ee Mungu.

Usiwasahau wanyonge.

13Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu?

Kwa nini anajiambia mwenyewe,

“Hataniita nitoe hesabu”?

14Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni,

umekubali kuyapokea mkononi mwako.

Mhanga anajisalimisha kwako,

wewe ni msaada wa yatima.

15Vunja mkono wa mtu mbaya na mwovu;

mwite mtu mbaya atoe hesabu ya uovu wake

ambao usingejulikana vinginevyo.

16Bwana ni Mfalme milele na milele,

mataifa wataangamia watoke nchini mwake.

17Unasikia, Ee Bwana , shauku ya wanaoonewa;

wewe huwatia moyo, na kusikiliza kilio chao,

18ukiwatetea yatima na waliodhulumiwa,

ili mwanadamu ambaye ni udongo asiogopeshe tena.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.