The chat will start when you send the first message.
1Ee Mwenyezi Mungu, mkumbuke Daudi
na taabu zote alizozistahimili.
2Aliapa kiapo kwa Mwenyezi Mungu
na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo:
3“Sitaingia nyumbani mwangu
au kwenda kitandani mwangu:
4sitaruhusu usingizi katika macho yangu,
wala kope zangu kusinzia,
5hadi nitakapompatia Mwenyezi Mungu mahali,
makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
6Tulisikia habari hii huko Efrata,
tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara:
7“Twendeni kwenye makao yake,
na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake;
8inuka, Ee Mwenyezi Mungu, uje mahali pako pa kupumzikia,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
9Makuhani wako na wavikwe haki,
watakatifu wako na waimbe kwa furaha.”
10Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako,
usimkatae mpakwa mafuta wako.
11Mwenyezi Mungu alimwapia Daudi kiapo,
kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua:
“Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe
kwenye kiti chako cha ufalme,
12kama wanao watashika agano langu
na sheria ninazowafundisha,
ndipo wana wao watakalia kiti chako cha ufalme
milele na milele.”
13Kwa maana Mwenyezi Mungu ameichagua Sayuni,
amepaonea shauku pawe maskani yake:
14“Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele;
hapa ndipo nitakapoketi nikitawala,
kwa sababu nimepaonea shauku:
15Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele:
nitashibisha maskini wake kwa chakula.
16Nitawavika makuhani wake wokovu,
nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha.
17“Hapa nitamchipushia Daudi pembe,[#132:17 pembe inawakilisha nguvu]
na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu.
18Adui zake nitawavika aibu,
bali taji kichwani pake litang’aa sana.”