The chat will start when you send the first message.
1Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
nimhofu nani?
2Waovu watakaposogea dhidi yangu
ili wale nyama yangu,
adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,
watajikwaa na kuanguka.
3Hata jeshi linizingire pande zote,
moyo wangu hautaogopa;
hata vita vitokee dhidi yangu,
hata hapo nitakuwa na ujasiri.
4Jambo moja ninamwomba Bwana ,
hili ndilo ninalolitafuta:
niweze kukaa nyumbani mwa Bwana
siku zote za maisha yangu,
niutazame uzuri wa Bwana
na kumtafuta hekaluni mwake.
5Kwa kuwa siku ya shida,
atanihifadhi salama katika maskani yake,
atanificha uvulini mwa hema lake,
na kuniweka juu kwenye mwamba.
6Kisha kichwa changu kitainuliwa
juu ya adui zangu wanaonizunguka.
Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;
nitamwimbia Bwana na kumsifu.
7Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana ,
unihurumie na unijibu.
8Moyo wangu unasema kuhusu wewe,
“Utafute uso wake!”
Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”
9Usinifiche uso wako,
usimkatae mtumishi wako kwa hasira;
wewe umekuwa msaada wangu.
Usinikatae wala usiniache,
Ee Mungu Mwokozi wangu.
10Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha,
Bwana atanipokea.
11Nifundishe njia yako, Ee Bwana ,
niongoze katika njia iliyo nyoofu,
kwa sababu ya watesi wangu.
12Usiniachilie kwa nia za adui zangu,
kwa maana mashahidi wa uongo
wameinuka dhidi yangu,
wakipumua ujeuri.
13Nami bado nina tumaini hili:
nitauona wema wa Bwana
katika nchi ya walio hai.
14Mngojee Bwana ;
uwe hodari na mwenye moyo mkuu,
na umngojee Bwana .