Zaburi 31

Zaburi 31

Zaburi 31

Maombi na sifa kwa kuokolewa kutoka kwa adui

1Ee Bwana , nimekukimbilia wewe,

usiache nikaaibika kamwe,

kwa haki yako uniokoe.

2Nitegee sikio lako,

uje uniokoe haraka;

uwe kwangu mwamba wa kimbilio,

ngome imara ya kuniokoa.

3Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu,

uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.

4Uniepushe na mtego niliotegewa,

maana wewe ndiwe kimbilio langu.

5Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,

unikomboe Ee Bwana , uliye Mungu wa kweli.

6Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili;

bali mimi ninamtumaini Bwana .

7Nitafurahia na kushangilia upendo wako,

kwa kuwa uliona mateso yangu

na ulijua maumivu ya nafsi yangu.

8Hukunikabidhi kwa adui yangu

bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.

9Ee Bwana unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;

macho yangu yanafifia kwa huzuni,

nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.

10Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,

naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;

nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,

na mifupa yangu inachakaa.

11Kwa sababu ya adui zangu wote,

nimedharauliwa kabisa na majirani zangu,

hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho,

wale wanaoniona barabarani wananikimbia.

12Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,

nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.

13Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi;

vitisho viko pande zote;

kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu,

na kula njama kuniua.

14Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Bwana ;

nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”

15Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,

uniokoe mikononi mwa adui zangu

na wale wanifuatiao.

16Mwangazie mtumishi wako uso wako,

uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.

17Usiniache niaibike, Ee Bwana ,

kwa maana nimekulilia wewe,

bali waovu waaibishwe

na kunyamazishwa Kuzimu.

18Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,

kwa maana kwa kiburi na dharau

wao husema kwa majivuno

dhidi ya wenye haki.

19Tazama jinsi wema wako ulivyo mkuu,

uliowawekea akiba wanaokucha,

unaowapa wale wanaokukimbilia

machoni pa watu wote.

20Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako

kutokana na hila za wanadamu;

katika makao yako huwaweka salama

kutokana na ndimi za mashtaka.

21Atukuzwe Bwana ,

kwa kuwa amenionesha upendo wake wa ajabu

nilipokuwa katika mji uliozingirwa.

22Katika hofu yangu nilisema,

“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”

Hata hivyo ulisikia kilio changu

ukanihurumia nilipokuita unisaidie.

23Mpendeni Bwana ninyi watakatifu wake wote!

Bwana huwahifadhi waaminifu,

lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.

24Kuweni hodari na mjipe moyo,

ninyi nyote mnaomtumaini Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.