The chat will start when you send the first message.
1Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu
na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi;
nitaweka lijamu kinywani mwangu
wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”
2Lakini niliponyamaza na kutulia,
hata pasipo kusema lolote jema,
uchungu wangu uliongezeka.
3Moyo wangu ulipata moto ndani yangu,
nilipotafakari, moto uliwaka,
ndipo nikasema kwa ulimi wangu:
4“Ee Bwana , nijulishe mwisho wa maisha yangu
na hesabu ya siku zangu;
nijalie kujua jinsi maisha yangu
yanavyopita upesi.
5Umefanya maisha yangu mafupi kama nyanda;
muda wangu wa kuishi ni kama
hauna thamani kwako.
Maisha ya kila mwanadamu
ni kama pumzi.
6Hakika kila binadamu ni kama njozi
aendapo huku na huko:
hujishughulisha na mengi, lakini ni ubatili;
anakusanya mali nyingi,
wala hajui ni nani atakayejifaidi nayo.
7“Lakini sasa Bwana, nitafute nini?
Tumaini langu ni kwako.
8Niokoe kutoka makosa yangu yote,
usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.
9Nilinyamaza, sikufumbua kinywa changu,
kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.
10Niondolee mjeledi wako,
nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.
11Unakemea na kuadhibu wanadamu
kwa ajili ya dhambi zao;
unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo:
kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
12“Ee Bwana , usikie maombi yangu,
usikie kilio changu unisaidie,
usiwe kiziwi kwa kulia kwangu.
Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni,
mhamiaji, kama walivyokuwa baba zangu wote,
13Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena
kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”