The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,
uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.
2Unifiche kutokana na njama za waovu,
kutokana na fitina za kundi la watenda maovu.
3Wananoa ndimi zao kama panga
na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.
4Hurusha mishale kutoka mavizio kwa mtu asiye na hatia,
humrushia ghafula bila woga.
5Kila mmoja humtia moyo mwenzake
katika mipango mibaya;
huzungumza kuhusu kuficha mitego yao,
nao husema, “Ni nani ataiona?”
6Hupanga njama la dhuluma na kusema,
“Tumebuni mpango mkamilifu!”
Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.
7Bali Mungu atawapiga kwa mishale,
nao ghafula wataangushwa.
8Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao
na kuwaleta kwenye maangamizi;
wote wawaonao watatikisa vichwa vyao
kwa dharau.
9Wanadamu wote wataogopa,
watatangaza kazi za Mungu
na kutafakari yale aliyoyatenda.
10Wenye haki na wafurahi katika Bwana ,
na wakimbilie kwake;
wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!