The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, mjalie mfalme aamue kwa haki yako,
mwana wa mfalme kwa haki yako.
2Atawaamua watu wako kwa haki,
watu wako walioonewa kwa haki.
3Milima italeta mafanikio kwa watu,
vilima tunda la haki.
4Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu
na atawaokoa watoto wa wahitaji,
ataponda mdhalimu.
5Atadumu kama jua linavyodumu, kama mwezi, vizazi vyote.
6Atakuwa kama mvua inavyonyesha juu ya shamba lililofyekwa,
kama manyunyu yanavyonyeshea ardhi.
7Katika siku zake wenye haki watastawi;
mafanikio yatakuwepo hadi mwezi utakapokoma.
8Atatawala kutoka bahari hadi bahari
na kutoka Mto hadi miisho ya dunia.
9Makabila ya jangwani watamsujudia,
na adui zake wataramba mavumbi.
10Wafalme wa Tarshishi na wa pwani za mbali
watamletea ushuru;
wafalme wa Sheba na Seba
watampa zawadi.
11Wafalme wote watamsujudia
na mataifa yote yatamtumikia.
12Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia,
aliyeonewa asiye na wa kumsaidia.
13Atawahurumia wanyonge na wahitaji
na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti.
14Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili,
kwani damu yao ni ya thamani machoni pake.
15Aishi maisha marefu!
Na apewe dhahabu ya Sheba.
Watu wamwombee daima
na kumbariki mchana kutwa.
16Nafaka ijae tele katika nchi yote,
juu ya vilele vya vilima na istawi.
Tunda lake na listawi kama Lebanoni,
listawi kama majani ya kondeni.
17Jina lake na lidumu milele,
na lidumu kama jua.
Mataifa yote yatabarikiwa kupitia kwake,
nao watamwita aliyebarikiwa.
18Ahimidiwe Bwana Mungu, Mungu wa Israeli,
ambaye peke yake hutenda mambo ya ajabu.
19Jina lake tukufu lihimidiwe milele,
ulimwengu wote ujae utukufu wake.
20Huu ndio mwisho wa maombi ya Daudi mwana wa Yese.