Zaburi 94

Zaburi 94

Zaburi 94

Mungu, Mlipiza kisasi kwa ajili ya wenye haki

1Ee Bwana , ulipizaye kisasi,

Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.

2Ee Mhukumu wa dunia, inuka,

uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.

3Ee Bwana , hadi lini waovu,

hadi lini waovu watashangilia?

4Wanamimina maneno ya kiburi,

watenda maovu wote wamejaa majivuno.

5Ee Bwana , wanawaponda watu wako;

wanawatesa walio urithi wako.

6Wanamchinja mjane na mgeni,

na kuwaua yatima.

7Nao husema, “Bwana haoni,

Mungu wa Yakobo hafahamu.”

8Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu;

enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?

9Je, aliyeweka sikio asisikie?

Aliyeumba jicho asione?

10Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?

Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?

11Bwana anajua mawazo ya mwanadamu;

anajua kwamba ni ubatili.

12Ee Bwana , heri mtu anayeadhibishwa na wewe,

mtu unayemfundisha kwa sheria yako,

13unampa utulivu siku za shida,

hadi shimo litakapokuwa limechimbwa

kwa ajili ya mwovu.

14Kwa kuwa Bwana hatawakataa watu wake,

hatauacha urithi wake.

15Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,

wote walio na mioyo minyofu wataifuata.

16Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?

Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?

17Kama Bwana hangenisaidia upesi,

ningeishi katika kimya cha kifo.

18Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

Ee Bwana , upendo wako ulinishikilia.

19Wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

20Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,

ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?

21Huungana kuwashambulia wenye haki,

kuwahukumu kufa wasio na hatia.

22Lakini Bwana amekuwa ngome yangu,

na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.

23Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao

na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;

Bwana Mungu wetu atawaangamiza.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.