Waamuzi 18

Waamuzi 18

Kuhama kwa Dani

1Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila la Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hawakuwa wamepata urithi wao kati ya makabila ya Israeli.[#Amu 17:6; 21:25; Yos 19:47]

2Basi wana wa Dani wakatuma watu watano kutoka kwa koo zao zote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuikagua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hadi nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko.[#Amu 13:25; Hes 13:17; Yos 2:1; Amu 17:1]

3Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo kijana Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda huko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Unafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa?

4Naye akawaambia, Hivi na hivi, ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake.[#Amu 17:10; Yn 10:12,13; Mdo 18:18,21; 20:33; 1 Tim 3:3; Tit 1:11; 2 Pet 2:3]

5Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kama njia yetu tuiendeayo itafanikiwa.[#1 Fal 22:5; Hos 4:12; Amu 17:5]

6Kuhani akawaambia, Haya nendeni na amani; njia mnayoiendea iko mbele za BWANA.[#1 Fal 22:6]

7Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa kwa amani, kama ilivyokuwa desturi ya Wasidoni, watu watulivu na wasioshuku, wasiopungukiwa na chochote duniani, na waliokuwa na miliki; Nao walikuwa mbali na hao Wasidoni, wala hawakutangamana na watu wengine.[#18:7 Linganisha na 18:10. Maana katika Kiebrania si dhahiri.; #18:7 Maana katika Kiebrania si dhahiri.]

8Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani?

9Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Hamtafanya chochote? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo.[#Hes 13:20; 14:7-9; Yos 2:23,24; 1 Sam 14:48; 1 Fal 22:3]

10Hapo mtakapokwenda mtawafikia watu wakaao kwa amani, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapapungukiwi na kitu chochote kilichoko duniani.[#Kum 8:9]

11Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli.

12Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu.[#Yos 15:60; #18:12 Maana yake ni Kambi ya Dani.]

13Nao wakapita huko hadi hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakaifikia nyumba ya huyo Mika.

14Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakawaambia ndugu zao, Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasavyo kufanya.[#1 Sam 14:28; Amu 8:27; 17:5; 1 Sam 23:6]

15Basi wakageuka wakaenda huko, wakafika katika nyumba ya huyo kijana Mlawi, huko nyumbani kwa Mika, kumwamkia.[#Mwa 43:27; 1 Sam 17:22]

16Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.

17Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao wanaume mia sita wenye kuvaa silaha za vita.[#Mwa 31:19,30; Amu 6:31; 17:4,5; 2 Fal 19:18; Isa 41:29; 46:12; Mik 5:13]

18Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?

19Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?[#Ayu 21:5; 29:9; Mit 30:32; Mik 7:16; Mwa 45:8; Amu 17:10; 2 Fal 6:21; 13:14; Isa 22:21; Mt 23:9]

20Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu.

21Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa kufugwa, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao.

22Walipokuwa wamekwenda mbali kidogo kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani.

23Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?

24Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?

25Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikike kati yetu, wasije walio na hasira wakakupiga, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako.[#2 Sam 17:8]

26Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa wanamzidi nguvu, akageuka akarudi nyumbani kwake.

Wadani wafanya makao katika Laisha

27Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafika Laisha, kwa watu waliokuwa watulivu na wasioshuku, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakauteketeza kwa moto mji wao.[#Kum 33:22; Yos 19:47]

28Wala hakukuwa na mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa mbali sana na Sidoni, nao hawakutangamana na watu wowote wale; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.[#Mwa 49:13; Yos 8:11; Amu 10:12; Hes 13:21; 2 Sam 10:6]

29Wakauita mji jina lake Dani, kwa kulifuata jina la baba yao Dani, aliyezaliwa na Israeli; lakini jina la mji huo hapo awali lilikuwa Laisha.[#Yos 19:47; Mwa 14:14; Amu 20:1; 1 Fal 12:29; 15:20]

30Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila la Wadani hadi siku nchi hiyo ilipochukuliwa mateka.[#Amu 13:1; 1 Sam 4:2; Zab 78:60]

31Basi wakaiabudu hiyo sanamu ya kuchonga aliyotengeneza Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.[#Yos 18:1; 1 Sam 4:1]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania