Zaburi 132

Zaburi 132

Maskani ya milele ya Mungu katika Sayuni

1BWANA, umkumbukie Daudi

Taabu zake zote alizotaabika.

2Ndiye aliyemwapia BWANA,

Akaweka nadhiri kwa shujaa wa Yakobo.

3“Sitaingia nyumbani mwangu,

Wala sitalala kitandani mwangu;

4Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi,[#Rut 3:18]

Wala kope zangu kusinzia;

5Hadi nitakapompatia BWANA mahali,

Na Mwenye nguvu wa Yakobo maskani”.

6Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,[#Yos 18:1; 1 Nya 13:5; 2 Nya 6:41-42; 1 Sam 17:12; 7:1]

Katika shamba la Yearimu tuliiona.

7Na tuingie katika maskani yake,

Tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake.

8Ee BWANA, uinuke, uende kwenye raha yako,[#Hes 10:35]

Wewe na sanduku la nguvu zako.

9Makuhani wako na wavikwe haki,[#Ayu 29:14; Isa 61:10]

Watauwa wako na washangilie.

10Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,

Usiurudishe nyuma uso wa masihi wako.

11BWANA amemwapia Daudi neno la kweli,[#1 Fal 8:25; 2 Sam 7:12-16; 1 Nya 6:16; 17:11-14; Zab 89:4-5; Lk 1:69; Mdo 2:30]

Hatarudi nyuma akalivunja,

Mmoja wa wana wako mwenyewe

Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.

12Wanao wakiyashika maagano yangu,

Na shuhuda nitakazowafundisha;

Watoto wao nao wataketi

Katika kiti chako cha enzi milele.

13Kwa kuwa BWANA ameichagua Sayuni,

Ameitamani akae ndani yake.

14Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,

Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani.

15Hakika nitavibariki vyakula vyake

Wahitaji wake nitawashibisha chakula.

16Na makuhani wake nitawavika wokovu,[#2 Nya 6:41; Hos 11:12]

Na watauwa wake watashangilia.

17Hapo nitamchipushia Daudi pembe,[#1 Fal 11:36; Zab 92:10; Eze 29:21; Lk 1:69]

Na taa nimemtengenezea masihi wangu.

18Adui zake nitawavika aibu,

Bali juu yake taji lake litasitawi.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania